Powered by: Elbahsan Web & Blog Designer
Do want your Network!!! Website or Blog-Spot, Try Us: Elbahsan Web & Blog Designer Contact Us Now... Calll; +255743550360 | +255788680558 Email; murtadhaalbahsan@gmail.com

Zawamba Photo Production

Alhamisi, 15 Juni 2017

Tundu Lissu,Abdallah Mtolea Wapinga Azimio la Bunge Kumpongeza Rais Magufuli

Azimio la Bunge la kumpongeza Rais John Magufuli kwa hatua anazochukua kukabiliana na upotevu wa mapato ya serikali katika sekta ya madini jana liligawa Bunge baada ya wabunge wa upinzani kulikataa wakati wenzao wa CCM wakilikubali.

Mwenyekiti wa Bunge, Musa Zungu alipowahoji wabunge kama wanakubali azimio hilo, wabunge wote wa CCM waliitikia "ndiyooo" wakati wale wa upinzani walisema "siyooo".

Azimio hilo lenye kurasa mbili liliwasilishwa bungeni jana na Mbunge wa Newala Mjini (CCM), George Mkuchika na baada ya hapo wabunge walipata nafasi ya kulijadili.

“Bunge linamuunga mkono Rais John Magufuli na lipo tayari kutoa ushirikiano wa dhati kadri itakavyohitajika kuhakikisha juhudi hizi hazipotei bure na sekta ya madini inachangia maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla,” alisema Mkuchika ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Haki, Kinga, Maadili na Madaraka ya Bunge.

Lakini, aliposimama akiwa wa kwanza kuchangia hoja ya maazimio hayo, Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alipinga akisema ni kinyume na majukumu ya Bunge hivyo kulitaka lisiendelee na taratibu za kumpongeza Rais akisema alichokifanya si kipya.

“Kazi ya Bunge ni kuishauri Serikali, siyo kuipongeza au kuiimbia mapambio. Hili siyo azimio la Bunge, bali wana-CCM kumpongeza mwenyekiti wao,” alisema mnadhimu huyo wa Kambi ya Upinzani Bungeni.

Alisema kinachofanywa na Rais Magufuli kilifanywa pia na watangulizi wake waliounda tume kadhaa na kwamba mpaka azimio hilo linajadiliwa, bado usafirishaji wa dhahabu inayochimbwa kwenye migodi mbalimbali nchini unaendelea.

“Dhahabu na madini mengine yanaendelea kusafirishwa hivi sasa. Ripoti za Profesa Mruma na Profesa Osoro ni professorial rubbish. Ni uongo, uongo, uongo,” alisema Lissu.

Ingawa alitakiwa kufuta neno rubbish kwenye mchango wake, Lissu alifafanua kwamba ripoti za wenyeviti hao wa kamati mbili za Rais za kuchunguza makontena 277 ya mchanga wa dhahabu, hazina taarifa sahihi.

Kuhusu azimio hilo kutokuwa na jipya, alisema Rais mstaafu, Benjamin Mkapa aliunda kamati ya Jenerali (Robert) Mboma mwaka 2002, ya Dk (Jonas) Kipokola mwaka 2004 kisha ya Dk (Enos) Bukuku mwaka 2005. Alisema hata Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete naye aliunda mbili za Lawrence Masha na Jaji Mark Bomani.

Alisema kama Bunge linataka kupongeza kuhusiana na kamati zilizoundwa na Rais Magufuli, basi halina budi kuanza na watangulizi hao ambao walifanya kama anachokifanya sasa kwa masilahi ya Taifa huku akipendekeza semina itolewe kwa wabunge ili kuwaongezea uelewa wa masuala ya madini na kuwafanya wachangie wakiwa na ufahamu wa kutosha kuhusu sekta hiyo.

Lissu alipingwa na Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde ambaye alitoa sababu za kumpongeza Rais Magufuli akisema kuna tofauti kati ya kamati alizoziunda na zile za watangulizi wake.

“Rais ameenda mbali zaidi. Ripoti imepokewa hadharani na wananchi wote wameisikia. Hii ni hatua ya mbele. Haiwezekani Taifa lisimpongeze Rais anapofanya mambo yanayoonekana,” alisema.

Alisema ameona clip (video fupi) za mawaziri wakuu wastaafu waliohamia upinzani; Edward Lowassa na Frederick Sumaye wakimpongeza Rais kwa hatua zake.

Lakini, Mbunge wa Temeke (CUF), Abdallah Mtolea alionekana kuungana na Lissu akiongeza kwamba maazimio hayo hayakuwa sawa kwa maelezo kwamba kilichofanywa na Rais Magufuli mpaka sasa hakijapiga hatua kubwa zaidi ya kilichofanywa na watangulizi wake.

Alisema suala la msingi ni kudhibiti wizi wa rasilimali nchini akikumbusha kwamba Kikwete pia aliunda tume lakini hata baada ya kupelekewa ripoti, hakufanya chochote hatua ambayo Rais Magufuli amefikia mpaka sasa kwenye vita aliyoianzisha.

Alisema hoja ya wizi wa madini ilianzishwa siku nyingi na wabunge ambao walionekana kuwa si wazalendo. “Kama Mkapa na Kikwete tungewapongeza kwa kuunda tume leo ingekuwaje? Bunge tusiwe washangiliaji,” alisema.

Alikumbusha pia kwamba Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CCM), Peter Serukamba alipiga kelele, Dk Hamis Kigwangallah wa Nzega Vijijini (CCM) aliteswa, Tundu Lissu, Zitto Kabwe wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo) na John Mnyika wa Kibamba (Chadema) walilizungumza suala hilo lakini walibezwa.

Alisema kwa kuwa suala hilo sasa linazungumzwa na mtu anayependwa, linaungwa mkono.

Katika mchango wake, Hasunga ambaye ndiye aliyekuwa mtoa hoja alisema hatua ya Rais kuzuia usafirishaji wa mchanga nje ni muhimu inayopaswa kuungwa mkono na Watanzania wote.

“Jimboni na mkoani kwangu kuna madini mengi, hatustahili kuwa maskini,” alisema.

Akiunga mkono hoja hiyo, Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola alisema anachokifanya Rais Magufuli ndicho alichoahidi hata kabla hajashika wadhifa huo,

“Aliahidi watu watalima kwa meno, tunaona mafisadi wakilima kwa meno. Namuomba hata watu wanaowatetea wezi hawa awalimishe kwa meno pia.”

Mbunge huyo ambaye aghalabu huzungumza kwa mbwembwe aliungwa mkono na Mbunge wa Rufiji (CCM), Mohamed Mchengerwa ambaye alitaka neno uzalendo liondolewe kwenye kamusi ya Kiswahili endapo kuna mtu atapinga yanayofanywa na Rais Magufuli.

“Tunaamini mambo haya yakitekelezwa vyema tutakuwa na barabara za lami na hatutakuwa na deni la Taifa,” alisema Mchengerwa.

Serikali Yatoa Onyo.......Yavitaka vyombo vya habari kuacha kuwahusisha Marais wastaafu na mchanga wa madini

Serikali ya Tanzania kupitia Waziri ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imevitaka vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuacha kuwatuhumu Marais wastaafu kwenye sakata la mchanga wa madini kwani majina yao hayajatajwa kwenye ripoti ambayo Rais Magufuli ameipokea.

Katika taarifa ambayo imetolewa na Waziri Mwakyembe imeeleza kuwa kuna baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii wamekuwa wakituhumu Marais wastaafu bila kujua athari zake kiasiasa na kijamii 
 

Viongozi wa Dini Watangaza Siku Saba za Kumwombea Rais Magufuli

Na Jonas Kamaleki- MAELEZO
Viongozi wa dini wametangaza maombi ya siku saba nchi nzima kumwombea Rais John Pombe Magufuli ili aendelee na juhudi zake za kulinda raslimali za watanzania kwa manufaa ya Taifa kwa ujumla.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam katika mahojiano maalum na Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu kwa jamii ya dini zote, Askofu William Mwamalanga kwa niaba ya viongozi wa dini.

“Tumeamua kufanya maombi ya siku saba kwa kumtaka kila mtanzania popote alipo kutembea hatua saba kila siku akimwombea Mhe. Rais Magufuli ili Mungu amlinde pamoja na anaofanyanao kazi kwa usahihi (uaminifu)”, alisema Askofu Mwamalanga.

Ndani ya siku hizo saba kila mtanzania atakuwa ametembea jumla ya hatua 49 akimwombea Rais Magufuli na wazalendo wenzake.

Kwa mujibu wa Kiongozi huyo wa Dini, maombi hayo yataanza leo Alhamisi Juni 15 nchi nzima na yatajumuisha watu wa dini zote nchini, yaani madhehebu ya Kiislam, Kikristo, Kihindu, Budha na madhehebu mengine.

Maombi haya yanafanyika baada ya kuona kuwa Mhe. Rais Magufuli anachukua hatua madhubuti za kutaka waliohusika kwa namna yoyote kuiba raslimali za Taifa hususani madini, wanachukuliwa hatua na kuitaka kampuni ya ACCASIA kulipa kile ambacho walichukua kinyume cha sheria.

Askofu Mwamalanga alisema kuwa Kamati yake inamwomba Rais Magufuli achukue hatua za haraka kudhibiti raslimali za nchi kwa upande wa Wizara ya Maliasili na Utalii ambako mali nyingi zinatoroshwa na wajanja wachache.

Kamati hiyo ya Kitaifa ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu kwa jamii ya dini zote imemwomba Mhe. Rais aziunganishe Wizara za Nishati na Madini na Maliasili na Utalii na kuunda wizara moja ambayo itasimamia kwa karibu raslimali za watanzania.

“Tunamwomba Rais Magufuli amchague mtu makini na mzalendo mwenye uchungu na nchi hii ili asimamie wizara hiyo, na nina hakika wizara hiyo ikisimamiwa vizuri, ndoto ya Rais ya kuifanya Tanzania kuwa nchi mhisani itatimia kwa kuwa hapa Mungu ametujalia kila kitu”,alisema Askofu Mwamalanga.

Viongozi hao wamempongeza Rais Magufuli kwa Uzalendo na Ujasri alionao katika kulinda raslimali za Taifa na kupambana na maovu. Wamesema ni kiongozi wa kuigwa na Marais au viongozi Duniani kote.

Kuhusu suala la walioachishwa kazi kutokana na kuwa na vyeti feki, Askofu Mwamalanga alisema kuwa Kamati inamwomba Mhe Rais kuwasamehe wale ambao wameitumikia nchi hii kati ya miaka mitano na 30 ili walau wapatiwe kifuta jasho licha ya kwamba walitumika bila kuwa na vyeti halali vya Kidato cha nne.

“Msamaha tunaoomba si wa kuwarudisha kazini bali tunaomba kwa ajili ya kupata kiinua mgongo kwani wengine walitumika kwa uaminifu na hata kupewa tuzo za ufanyakazi hodari (bora) hasa katika sekta za Afya,wauguzi, Elimu na maeneo mengine”, alisema Askofu Mwamalanga.

Mapema wiki hii, Rais Magufuli alipokea ripoti ya pili ya uchunguzi wa makinikia ambayo iliwajumuisha wanasheria na wachumi. Katika ripoti hiyo ilibainika kuwa kiasi kikubwa cha madini kilichukuliwa bila watanzania kupata chochote. Takriban madini yenye thamani ya shilingi trilioni 108 yalisafirishwa nje ya nchi bila Tanzania kupata faida kutokana na madini hayo.

UKATILI: Msichana Asimulia Jinsi Kondakta na Dereva Walivyombaka Kwa Zamu Ndani ya Daladala

Dereva na kondakta wa daladala zinazofanya safari ndani ya Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Soweto–Mbuyuni wanatuhumiwa kumbaka abiria wao kwa zamu na kumuumiza sehemu za siri.

Tukio hilo lililotokea Juni 12 saa moja jioni maeneo ya Veta katika uchochoro uliopo karibu na shule ya Northen Highland iliyo umbali wa mita 400 kutoka barabara ya lami.

Akielezea tukio hilo, binti huyo mwenye umri wa miaka 20 alisema alitumwa na bosi wake kwenda kununua mahitaji ya nyumbani Soko la Mbuyuni na kumuelekeza kuwa akimaliza apande basi la Soweto sokoni hapo na ashukie mwisho ambako angechukua bodaboda ya kumfikisha nyumbani.

“Nilipomuuliza konda akaniambia ndiyo na nikampigia bodaboda ambaye nilipewa namba na bosi wangu ili ampe maelekezo huyo kondakta sehemu ambayo watanishusha ili yeye anichukue hapo na wakazungumza na baadaye akanirejeshea simu yangu,” alisema msichana huyo.

Alisema baada ya hapo safari ya kutoka Mbuyuni kwenda Soweto ilianza.

“Kwa kuwa nilikuwa mgeni, sikuelewa hata kituo kipi cha kushukia. Niliendelea kukaa hadi nilipoona watu wote wameisha kwenye (Toyota) Hiace, ndipo nikamuuliza konda kwa nini hanishushi akasema bado sijafika,” alisema.

Anasema alishangaa kuona dereva anaenda kuegesha gari uchochoroni na aliposimama, kondakta akashuka, akidai anaenda kujisaidia. “Aliporudi kwanye gari alifunga mlango na wakazima taa na kuanza kuniambia kuwa wamenipenda kama ninataka kuwa hai nikubaliane na wanachokitaka na nikikataa wataniua,” alisema binti huyo.

Alisema baadaye dereva alitoka kwenye usukani na kumfuata alipokaa na kuanza kumpapasa.

Alisema alipoona hivyo alijaribu kutoka nje kupitia dirishani, lakini walimvuta ndani huku wakimfunga mdomo asipige kelele na kumtishia kumuua.

“Nilikubali yaishe na nikatulia. Akaanza dereva huku kondakta akinishika mikono na baada ya kumaliza alichofanya, konda naye akaja akafanya hivyohivyo. Nilisikia maumivu, lakini nilishindwa kupiga kelele kwa kuwa walinitisha kuwa wangeniua,” alisema dada huyo.

“Walipomaliza kufanya ukatili huo, konda alimwambia dereva kuwa waniue kwa kuwa nimeshawatambua, lakini dereva akasema hakuna haja.”

Alisema katika mabishano hayo alijikaza na kuwaambia kuwa yeye ni mgeni na hajui popote kwa hiyo hatamwambia mtu kwa kuwa hilo ni tukio la aibu.

“Walikubaliana na mimi na wakaniambia kuwa ni kweli kubakwa ni kitendo cha aibu kwa hiyo nikimwambia mtu nitatengwa na jamii. Nikawaomba wanisaidie sehemu ya kupata msaada niweze kufika nyumbani,” alisema.

Alisema baadaye aliwaomba aende kuchukua kiatu chake kilichokuwa kimedondoka dirishani wakati akitaka kuruka, na walipomruhusu akatumia nafasi hiyo kusoma namba za gari.

Mlezi wake, Abdi Massawe alisema baada ya kufika nyumbani akiwa na bodaboda, binti huyo alimweleza tukio hilo na akatoa taarifa polisi ambako alipewa fomu ya matibabu aliyoitumia Hospitali ya Mawenzi, ambako vipimo vilithibitisha kuwa alibakwa.

“Huyu binti ni mgeni kutoka mkoani Singida. Hapa Moshi ana mwezi mmoja tu,” alisema Masssawe.

Massawe alisema baada ya hapo alianza kusaka daladala hilo kwa kutumia namba alizopewa na binti huyo na kufanikiwa kuikuta maeneo ya Soweto. Baadaye aliwapigia simu polisi ambao walifika na kushusha abiria waliokuwamo na kuipeleka kituoni.

Alisema wakati dereva akiendelea na mahojiano kondakta alitoroka.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Koka Moita alisema derava wa gari hilo aliyemtaja kuwa ni Salimu Abdalla (30) anashikiliwa na polisi ambao wanaendelea kumtafuta kondakta ambaye alitoroka akiwa katika kituo cha polisi.

Kwa sasa binti huyo anatibiwa Hospitali ya Mawenzi.

Jumanne, 13 Juni 2017

Prof. Muhongo, Andrew Chenge na Wahusika Wengine Wazuiwa kutoka nje ya Mipaka ya Tanzania

Serikali imeagiza, Mawaziri, Wanasheria Wakuu wa Serikali na Manaibu wao, Wakurugenzi wa idara za mikataba, na Makamishna wa madini, wanasheria wa Wizara ya Nishati na Madini na watumishi wengine wa Serikali na watu wote waliohusika katika kuingia mikataba ya uchimbaji madini, utoaji wa leseni za uchimbaji wa madini na kuongeza muda wa leseni, watumishi na wamiliki wa makampuni ya madini kuto toka nje ya mipaka ya Tanzania.

Agizo hilo lilitolewa jana  na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba ambaye alisema kuwa, wote waliotajwa kuhusika katika kulisababishia taifa hasara kupitia sekta ya madini, hawaruhusiwi kutoka nje ya mipaka ya Tanzania isipokuwa kwa kibali maalum kutoka serikalini.

“Naelekeza wote waliotajwa kuhusika hakuna kutoka nje ya mipaka ya nchi yetu isipokuwa kwa kibali maalum kutoka serikalini. Vyombo vitekeleze maagizo ya Rais kwa utimamu,” aliandika Waziri Nchemba kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Agizo hili limekuja ikiwa ni saa chache tangu Rais Magufuli alipoagiza kuwa, viongozi wote na watumishi mbalimbali waliohusika katika kusaini mikataba mibovu na kushiriki kwa namna yoyote ile, wahojiwe.

Miongoni mwa watakaoathiriwa na zuio hilo, ni pamoja na Maafisa wa TRA, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Andrew Chenge, Mwanyika, na Werema, Mkurugenzi Idara ya Mikataba, Mary Ndosi, Kamishna Dalali Peter Kafumu, Waziri Prof. Muhongo, Waziri Daniel Yona, Waziri Nazir Karamagi, Jaji Julius Malaba, Waziri William Ngeleja.

Awali Waziri Nchemba alimpongeza Rais Magufuli kwa jitihada alizozichukua katika kuhakikisha analinda rasilimali za wanyonge na kusema kuwa hakuna uzalendo kama huo.

“Hakuna uzalendo zaidi ya kulinda rasilimali za Taifa, Hakuna utetezi wa wanyonge zaidi ya kulinda rasilimali zao.Hongera sana Mh.Rais kwa uzalendo wa vitendo kwa Taifa letu.”