Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe
26 Novemba, 2018 ameungana na Maaskofu, Mapadre, Watawa na Waumini wa
Kanisa Katoliki kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Askofu wa Jimbo
Katoliki la Mbeya Mhashamu Askofu Evaristo Chengula aliyefariki dunia
tarehe 21 Novemba, 2018 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Jijini
Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa Matibabu.
Misa
Takatifu ya kumuaga Marehemu Askofu Chengula iliyoongozwa na Askofu
Mkuu Mwandamizi Jude Thadaeus Ruwa’ichi, imefanyika katika Kanisa la
Mtakatifu Imakulata lililopo Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu, Kurasini
Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu
Mhe. Benjamin William Mkapa na Mkewe Mhe. Mama Anna Mkapa.
Akizungumza
baada ya Misa hiyo Mhe. Rais Magufuli ametoa salamu za pole kwa
Maaskofu wote wa Kanisa Katoliki, Mapadre, Watawa, Waumini wa Kanisa
Katoliki Jimbo la Mbeya na Wakatoliki wote nchini kwa kuondokewa na
kiongozi aliyekuwa akifanya vyema kazi yake ya kutangaza Injili.
Mhe.
Rais Magufuli amesema pamoja na majukumu yake ya kutoa huduma za kiroho
Marehemu Askofu Chengula alisimamia ukweli ikiwemo kupinga hadharani
ndoa na mapenzi ya jinsia moja licha ya kuwepo mashinikizo mbalimbali.
Akitoa
salamu kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) Makamu wa Rais wa
TEC Mhashamu Askofu Flavian Kasalla amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa
ushirikiano alioutoa wakati wa kuuguza na baada ya kifo cha Askofu
Chengula na pia amewashukuru madaktari na wauguzi, viongozi na wote
waliokuwa wakimuombea kabla na baada ya kifo.
Mhashamu
Askofu Evaristo Chengula amefariki dunia kwa ugonjwa wa moyo na baada
ya Misa ya kumuaga mwili wake umesafirishwa kwenda Mbeya.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
26 Novemba, 2018
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni