MZEE NGUNGA AFARIKI DUNIA
PENGO LAKE HALITAZIBIKA
NI VETERANI SKAUTI ALIYEKABIDHIWA SKAUTI NA WAKOLONI
Chama cha Skauti Tanzania (TSA) kimepatwa na pigo lingine la kuondokewa na kipenzi chake aliyeanza Skauti tangu enzi ya Ukoloni.
Marehemu
Ndugu Isdor Stanslaus Ngunga alizaliwa tarehe 12 Januari 1928 katika
kijiji cha Mwenge Mshindo, Wilaya ya Songea, Mkoa wa Ruvuma na alijiunga
katika Chama cha Skauti Tanzania Mkoa wa Ruvuma mwaka 1940 akiwa ni
mwanafunzi katika shule ya Mtakatifu Benedict (Father Benedict Middle
School) iliyopo Peramiho Mkoani Ruvuma.
Marehemu Mzee Isdor Stanslaus Ngunga, enzi ya uhai wake akiwa nyumbani kwake alipotembelewa na waandishi wa Dar Scout Media kwa mahojiano. |
Marehemu alipenda sana
mafunzo ya Skauti na kuendelea nayo hadi alipojiunga na Elimu ya juu
katika Chuo hicho hicho cha Mtakatifu Benedict, Peramiho.
Marehemu Mzee Ngunga alipata mafunzo mbalimbali ya Skauti ndani na nje ya nchi.
- Alipata Mafunzo ya Mwanzo ya Uongozi (PTC) mwaka 1950
- Mafunzo ya Skauti (Wood Badge - WB) mwaka 1955.
UONGOZI
Amewai kushika nafasi
mbali mbali za uongozi ambapo mwaka 1955 aliteuliwa kuwa Kiongozi wa
Skauti, yaani "Scout Master" wa kundi la Skauti la Litembo mjini Songea.
- Mwaka 1960 aliteuliwa kuwa Kiongozi wa Skauti wa Wilaya (District Scout Master) katika Wilaya ya Songea.
- Mwaka 1961 aliteuliwa kuwa "Field Commissioner" Makao Makuu ya Chama cha Skauti Tanzania.
- Mwaka 1979 aliteuliwa kuwa Kamishna Mkuu Msaidizi wa Mafunzo Tanzania.
- Mwaka 1994 aliteuliwa kuwa Kamishna Mkuu Msaidizi Mambo ya Nje.
- Mwaka 1992 aliteuliwa kuwa Naibu Kamishna Mkuu Tanzania.
- Mwaka 1998 aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mafunzo katika Chama cha Skauti Tanzania.
- Mwaka 2008 hadi mauti yake aliteuliwa kuwa Mshauri wa Chama cha Skauti Tanzania.
Skauti wakiwa wamebeba sanduku la mwili wa Marehemu Mzee Ngunga kutoka nyumbani kwake Kijitonyama barabara ya Akachube kuelekea Kanisani kwa maombi, tarehe 17 Juni 2015 siku ya Jumatano. |
Marehemu Ndugu Isidori
Ngunga katika shughuli zake za kazi kama Mwalimu katika Chuo cha Ualimu
Peramiho na baadae Nangosho Mbambabay, Seminary ya Kigonsera, Litembo na
Mtyangimbole huko Ruvuma aliendelea na shughuli za Skauti, shughuli
ambazo alizipenda na pia alifurahi kuona wanafunzi wake wengi wakijiunga
na Chama cha Skauti.
KUTOKA WIZARANI HADI SKAUTI
Akiwa ni Mtumishi wa
Wizara ya Elimu mara baada ya Nchi yetu kupata Uhuru mwaka 1961,
Marehemu Ndugu Isidori Stanslaus Ngunga aliazimwa kutoka Wizara ya Elimu
na kufanya kazi kama Field Commissioner katika Chama cha Skauti
Tanzania Makao Makuu, kazi ambazo zilimlazimu kusafiri ndani na nje ya
nchi, alifanya shughuli za Skauti katika mikoa ya Shinyanga, Dar es
Salaam na baadae Lagoni nchini Nigeria.
Kati ya mwaka 1975 hadi
1978 Marehemu Ndugu Isidori Ngunga aliteuliwa na Wizara ya Elimu
kuwafundisha Wakufunzi wa Umoja wa Vijana wa TANU/CCM mafunzo ya
Ujasiri na Maarifa na kuwafanya wawe wakakamavu kama vijana wa Skauti.
Mwaka 1974 hadi 1993 Marehemu
Ndugu Isidori Stanslaus Ngunga katika kutimiza majukumu yake ya kikazi
kama Mwalimu katika shule za Sekondari Jangwani na Mtakatifu Anthony
zote za Jijini Dar Es Salaam aliendelea na Skauti kwa wakati huo akiwa
ni Mshauri na Mkufunzi wa Chama cha Skauti Tanzania Makao Makuu.
Marehemu Ndugu Isidori
Stanslaus Ngunga atakumbukwa daima na Uongozi wa Skauti na Ma-Skauti
ndani na nje ya nchi kutokana utendaji wake mahiri na usimamizi mzuri wa
Program za vijana na viongozi wa Skauti kwa ujumla.
Aidha Marehemu
Ndugu Isidori Stanslaus Ngunga alishiriki kikamilifu katika shughuli ya
marekebisho ya Katiba mpya ya Chama cha Skauti Tanzania, Katiba ambayo
hadi hivi sasa bado ipo katika hatua za mwisho.
Baadhi ya Skauti wakiwa katika maombi katika kaburi la Marehemu Mzee Isidori Ngunga. |
Skauti wakiwasha mishumaa katika kaburi la Marehemu Ngunga |
Marehemu Ndugu Isidori
Stanslaus Ngunga alikuwa Mtunzi na Mwandishi wa Vijarida mbalimbali vya
Mafunzo ya Skauti na kama Chama tunaahidi kuendeleza pale alipoishia.
Chama cha Skauti
Tanzania tutamkumbuka daima Marehemu Veterani, Skauta, Mkufunzi na
Mshauri wa Chama cha Skauti Tanzania ambaye ametutoka ghafla, pengo
ambalo litachukua muda mrefu kuzibika.
Chama cha Skauti
Tanzania tumempoteza Kiongozi mahiri, hodari, Shupavu na Mchapakazi,
ambaye tutamkumbuka na kuenzi jina lake daima.
Sisi sote tulimpenda, lakini MUNGU amempenda zaidi.
Viongozi wa Skauti mbalimbali walikuwepo katika mazishi ya Marehemu Mzee Isidori Ngunga |
Padri akiongoza misa ya kumuombea Marehemu Mzee Ngunga, Kanisani RC Mwananyamala. |
Skauta Kiluswa akitoa heshima yake ya mwisho kwa Marehemu Mzee Ngunga, nyumbani kwa marehemu Kijitonyama, Jijini Dar Es Salaam. |
Kamishna Mtendaji Ndugu Eline Kitaly akitoa heshima yake ya mwisho kwa Marehemu Mzee Ngunga, nyumbani kwa marehemu Kijitonyama, Jijini Dar Es Salaam. |
BURIANI Prof. Isidori Stanslaus Ngunga12-01-1928 --- 07-06-2015 |
TUNAMUOMBA MWENYEZI MUNGU AIPUMZISHE ROHO YAKE MAHALI PEMA PEPONI.
AMEEN.
Habari hii kwa msaada wa Chama cha Skauti Tanzania
Kwa
habari zaidi ya mahojiano ya Marehemu Ndugu Isdor Stanslaus Ngunga na
Dar Scout Habari, yaliyofanyika 14 Julai 2014, picha na habari za
Viongozi wa Skauti, Skauti na chimbuko pamoja sababu ya Marehemu Ngunga
kuuitwa Professor wa Skauti Tanzania. Tembelea ukurasa huu tarehe 21
Juni 2015.
(c) Dar Scout Media, Scout Chat Forum 2015
This Blog Powerd by:
Elbahsan Web & Blog Designer
A Subsidiary of Elbahsan Web & Blog Designer for Global Development, Inc.
+255 (0) 653 373 432 & +255 (0) 778 246 889
For the Web & Blog Template and Designing
Dar Es Salaam, Tanzania
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni