Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba amesema mtu
aliyemtishia kwa bastola aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Nape Nnauye si askari wa Jeshi la Polisi, lakini
ameshapatikana na atashughulikiwa kwa mujibu wa utaratibu wa ulinzi na
usalama.
Mwigulu alisema hayo baada ya kufungua mkutano wa kazi wa
mwaka wa maofisa waandamizi wa polisi, makamanda wa mikoa na wakuu wa
vikosi wa Jeshi la Polisi ambao unafanyika mjini Dodoma. “Ameshapatikana (aliyemtishia Nape) na atashughulikiwa kwa
mujibu wa taratibu za ulinzi na usalama ambazo zimekuwa zikifanyika
ndani, lakini hazitangazwi,” alisema.
Hata hivyo, Mwigulu alikataa kuelezea kwa undani kuhusu mtu
huyo kwa kubainisha anatoka taasisi gani wala jina la mtuhumiwa kwa
madai kuwa ni kwa sababu ya usalama wake.
Mtu huyo alifanya kitendo hicho wakati Nape, ambaye alikuwa
Waziri wa Habari, alipokuwa anaelekea Hoteli ya Protea alikopanga
kuzungumza na waandishi wa habari baada ya mbunge huyo wa Mtama kuachwa
katika mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri.
Mtu huyo alikuwa pamoja na wenzake wawili ambao kwa pamoja
walikuwa wakimlazimisha arudi kwenye gari lake na kuondoka, lakini Nape
alibisha na ndipo mtu huyo aliporudi nyuma, kuchomoa bastola kutoka
kiunoni na kisha kumtishia kabla ya kutulizwa na mwenzake.
Watu hao walitoweka eneo hilo muda mfupi baadaye.
Siku moja baada ya tukio hilo Mwigulu alimwagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi, Ernest Mangu kumtafuta mtu huyo.
Mwigulu aliandika katika ukurasa wake wa twitter akisema:
“Mh Nape sio jambazi, hana record za uhalifu. Kitendo cha
kutolewa bastola si cha Kitanzania na si cha kiaskari. Nimemuagiza IGP
achukue hatua.” Tukio hilo lilitokea siku chache baada ya RC Paul Makonda
kuvamia kituo cha televisheni cha kampuni ya Clouds Media, akiwa na
askari wenye silaha za moto na kulazimisha arekodiwe mahojiano baina ya
watangazaji wa kipindi cha Shirika la Wambeya Duniani (Shilawadu) na
mwanamke anayedai kuzaa na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat
Gwajima, ambaye ameibukia kuwa mpinzani wa kiongozi huyo.
Hadi sasa, Jeshi la Polisi halijaeleza kuhusu askari hao waliojumuika kufanikisha uvamizi huo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni