Jeshi la Polisi mkoani Iringa linamshikilia mwenyekiti wa zamani wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu, kwa
tuhuma za kumshambulia mwanamke mmoja na kumsababishia maumivu makali
mwilini.
Msambatavangu, ambaye alikuwa miongoni mwa wanaCCM
waliofukuzwa uanachama katika Mkutano Mkuu Maalum wa chama hicho
uliofanyika mwezi Machi, alikamatwa jana mchana
Kamanda
wa Polisi mkoani Iringa, Julius Mjengi, alisema kuwa
kiongozi mstaafu anatuhumiwa kutenda kosa hilo wiki iliyopita.
Akifafanua,
Kamanda Mjengi alibainisha kuwa kiongozi huyo alitenda kosa hilo akiwa
na wenzake ambao asingeweza kuweka majina yao hadharani kwani
wanaendelea kuwatafuta.
"Ni kweli tunamshikilia Jesca
Msambatavangu, tumemkamata leo(jana) saa nane mchana na tunaendelea na
uchunguzi dhidi yake," alisema Mjengi na kuongeza:
"Jesca pamoja
na wenzake wanatuhumiwa kumshambulia mwanamke mmoja mkazi wa Kibwabwa,
walimshambulia na kisha kumchoma sindano ambayo mwanamke huyo hajui ni
ya kitu gani," alisema Mjengi.
Alipohojiwa zaidi, Mjengi alikataa
kuweka wazi jina la mwanamke na idadi ya watuhumiwa wengine kwa maelezo
kuwa kufanya hivyo kunaweza kuharibu upelelezi unaoendelea.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni