Wapinzani
wawili katika mgogoro wa uongozi wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad na
Profesa Ibrahim Lipumba sasa wamefikia pabaya baada ya kuamua kupambana
kuichukua ofisi ya makao makuu iliyopo Buguruni.
Kwa
sasa ofisi hiyo inatumiwa na Profesa Lipumba, ambaye uamuzi wake wa
kurejea madarakani mwaka mmoja baada ya kujiuzulu uenyekiti na nyadhifa
nyingine zote, unapingwa na kundi lililopanga kuzichukua ofisi hizo
Jumapili.
Jana,
kundi linalompinga Profesa Lipumba lilitangaza kuwa litakwenda ofisi
hizo Jumapili kwa ajili ya kusafisha “kila kitu ambacho hakitakiwi
kiwepo”, lakini mwenyekiti huyo amesema ameshajiandaa kukabiliana nao na
ameripoti suala hilo polisi.
Profesa
Lipumba alisema hayo jana, ikiwa ni siku moja tangu Jukwaa la Wahariri
Tanzania (TEF) limtake ajitokeze kuzungumzia kitendo cha walinzi wa CUF
kuwashambulia waandishi wa habari waliokuwa kwenye mkutano ulioandaliwa
na viongozi wa chama hicho Kinondoni.
Profesa
Lipumba alikuwa akiwajibu wabunge wa CUF wanaomuunga mkono Maalim Seif
waliowaambia wanahabari katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma jana kuwa
wamepanga kwenda ofisi za Buguruni Jumapili ijayo na wataungana na
wanachama wengine kufanya usafi.
“Tulianza
kufanya usafi soko la Buguruni, tukamalizia katika ofisi yetu. Kwa hiyo
katika hali nzuri, hatuhitaji wabunge wasumbuke kufanya usafi siku
hiyo,” alisema Profesa Lipumba
Profesa
Lipumba alisema watu hao hawana nia ya dhati ya kufanya usafi, bali
wamepanga kufanya vurugu katika ofisi hizo kwa kushirikiana na watu wa
chama kingine cha upinzani.
“Wanataka
kuleta vurugu ili CUF ionekane na taswira mbaya kwa Watanzania. Naomba
wanachama waepuke mtego huu, namshauri (Mbunge wa Temeke, Abdallah)
Mtolea akafanye usafi huo Temeke mbona kuna masoko mengi tu machafu?” alisema.
Awali mjini Dodoma, wabunge wanaomuunga Maalim Seif walisema watakwenda na vifaa vya usafikuondoa kila uchafu watakaoukuta
“Wanachama
wa Chama cha Wananchi (CUF) ambao hawamkubali Profesa Ibrahim Lipumba
kuwa mwenyekiti, wameamua kwenda kufanya usafi kwenye ofisi zao za
Buguruni, ofisi kuu ya CUF Buguruni,” alisema Mtolea akiwa ameambatana na wabunge wenzake katika mkutano na waandishi uliofanyika chumba cha habari cha Bunge.
“Na
hatua hii imekuja baada ya kuona ofisi ile inatumika vibaya. Imekuwa
ndio kijiwe cha wahuni kupanga matukio ya kihalifu. Kwenda kuvamia
mikutano, kwenda kuwavamia watu na kadhalika. Sasa sisi kama wanachama
tumeona hatuwezi kuiacha hali hiyo iendelee.”
Aliwataka wanachama kutoka maeneo ya Dar es Salaam, Pwani na mikoa mingine wafike kufanya usafi huo.
Alipoulizwa
aina ya uchafu wanaoenda kuuondoa, Mtolea alijibu “ni kitu chochote
ambacho hakiko mahali pake” na kwamba hata Profesa Lipumba hayuko mahali
pake.
“Tangu
Msajili amtambue Profesa Lipumba kuwa mwenyekiti, hatujawahi kwenda
katika ofisi yetu ya Buguruni, matokeo yake ofisi hiyo imekuwa na uchafu
mwingi na kuwa pango la wahuni,” alisema Mtolea.
Alipoulizwa uwezekano wa kutokea vurugu, Mtolea alisema hawajiandai kufanya fujo, bali kufanya usafi.
Kuhusu
kesi iliyopo mahakamani kuhusu mgogoro huo, alisema ile inapinga
msajili kumtambua Lipumba na haizuii kusafisha ofisi yao.
Alisema hawaendi kuteka ofisi hizo, bali wanakwenda kwenye ofisi zao hivyo hawahitaji kuomba ruhusa kwa mtu yeyote.
“Ofisi ni chafu, sisi tunataka tukaisafishe kwa sababu imekuwa sehemu ya kupanga mipango mibaya kwa mustakabali wa chama,” alisema.
Akiweka msisitizo wa jibu hilo, Mbunge wa Chambani, Yusuf Salim Hussein alisema hakuna silaha ya moto inayoshinda nguvu ya umma.
Awali,
wabunge hao walitoa tamko la kuunga mkono tamko la TEF kuhusu kulaani
kitendo cha wafuasi wa Profesa Lipumba kuwashambulia waandishi wa
habari.
Mnadhimu
wa chama hicho na Mbunge wa Malindi, Ally Salehe alisema TEF imetoa
tamko zito la kutaka waandishi wa habari kufanya kazi kwa usalama na
uhuru.
“Na isiwe TEF tu, tunataka watu wote waliokerwa na tukio hilo watoe tamko la kulaani,” alisema.
Kuhusu tamko la TEF, Profesa Lipumba alisema atatoa tamko kuhusu suala hilo ifikapo leo.
“Mimi
ni muumini wa demokrasia. Hapa ninavyoongea na wewe nipo katika hatua
ya mwisho ya kumalizia kuandika barua kuelekea TEF ambayo itafika kati
ya leo (jana) jioni au kesho,” alisema.
Hata hivyo, alisema mkurugenzi wa habari, uenezi na mawasiliano kwa umma, Abdul Kambaya alitoa tamko kuhusu tukio hilo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni