MBUNGE wa Mtama, Nape Nnauye (CCM) ameiomba serikali itoe
tamko kuhusu uwekaji wa alama ya X kwa sababu zimekuwa zikikaa kwa muda
mrefu na kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi.
Mbunge huyo alitoa ombi hilo bungeni alipopewa nafasi na Spika Job Ndugai kuuuliza swali la nyongeza.
Katika maelezo ya utangulizi ya swali lake, Nape alisema
utaratibu wa kuweka alama ya X kwenye nyumba umezagaa nchi nzima na
unaathiri maendeleo ya wananchi.
Alisema utaratibu huo unazuia wananchi kuendeleza maeneo yao na inachukua muda mrefu kwa serikali kuanza kutekeleza mipango yao.
“Je, serikali haioni sasa umefika wakati wa kubadilisha
utaratibu huu... wawe wanapanga mipango yao, wakikamilisha ndiyo waende
kuzungumza na wananchi kwenye maeneo husika na kuweka alama hizo. “Mfano
mzuri ni kwenye maeneo ya Jimbo langu la Mtama ambapo inasemekana kuwa
utapita mradi wa reli na nyumba zimewekwa alama ya X kwa muda mrefu. Kama serikali itakubaliana na mpango huu itoe tamko hapa
ili niwaambie wananchi wangu wapake chokaa zile alama za X ili waendelee
na shughuli nyingine,” alisema.
Katika majibu yake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Edwin Ngonyani alisema serikali itaendelea kuziwekea alama
za X nyumba zote ambazo zimejengwa ndani ya hifadhi za barabara.
Katika swali la msingi la Mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilago
(CCM) alitaka kujua ni wananchi wangapi wa Wilaya ya Kakonko kati ya hao
wenye alama ya X wanaokidhi vigezo vya kulipwa na sababu ni zipi kwa
wasiolipwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni