Aliyekuwa
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu amewataka wananchi
kumpa ushirikiano IGP mpya, Simon Sirro katika kukabiliana na matukio ya
uhalifu nchini hasa katika Mkoa wa Pwani.
Mangu
aliyasema hayo jana Ikulu jijini Dar es salaam baada ya Rais John
Magufuli kumwapisha Sirro kuwa IGP mpya wa kuliongoza jeshi la polisi
nchini.
Kuhusiana na hali inayoendelea mkoani Pwani, Mangu alisema "Sirro
anafahamu anachotakiwa kufanya katika hilo, nimefanya naye kazi kwa
karibu, ninachoomba ni askari na wananchi wote wampe ushirikiano"
Mangu
ambaye anasubiri kupangiwa kazi nyingine alisema anamfahamu Sirro kama
mchapakazi mzuri na ataweza kutekeleza majukumu yake ya kuhakikisha
kwamba Tanzania inakuwa na amani.
Sirro aliapishwa jana kuwa IGP, kabla ya uteuzi huo alikuwa kamanda wa polisi (RPC) katika mikoa ya Tanga, Mwanza na Shinyanga.
Baadaye
alikwenda kitengo cha operesheni na mafunzo polisi makao makuu, kisha
akahamishiwa kitengo hicho kanda maalumu ya Dar es Salaam kabla ya kuwa
kamishna wa kanda hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni