Azimio
la Bunge la kumpongeza Rais John Magufuli kwa hatua anazochukua
kukabiliana na upotevu wa mapato ya serikali katika sekta ya madini jana
liligawa Bunge baada ya wabunge wa upinzani kulikataa wakati wenzao wa
CCM wakilikubali.
Mwenyekiti
wa Bunge, Musa Zungu alipowahoji wabunge kama wanakubali azimio hilo,
wabunge wote wa CCM waliitikia "ndiyooo" wakati wale wa upinzani
walisema "siyooo".
Azimio
hilo lenye kurasa mbili liliwasilishwa bungeni jana na Mbunge wa Newala
Mjini (CCM), George Mkuchika na baada ya hapo wabunge walipata nafasi
ya kulijadili.
“Bunge
linamuunga mkono Rais John Magufuli na lipo tayari kutoa ushirikiano wa
dhati kadri itakavyohitajika kuhakikisha juhudi hizi hazipotei bure na
sekta ya madini inachangia maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla,” alisema Mkuchika ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Haki, Kinga, Maadili na Madaraka ya Bunge.
Lakini,
aliposimama akiwa wa kwanza kuchangia hoja ya maazimio hayo, Mbunge wa
Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alipinga akisema ni kinyume na
majukumu ya Bunge hivyo kulitaka lisiendelee na taratibu za kumpongeza
Rais akisema alichokifanya si kipya.
“Kazi
ya Bunge ni kuishauri Serikali, siyo kuipongeza au kuiimbia mapambio.
Hili siyo azimio la Bunge, bali wana-CCM kumpongeza mwenyekiti wao,” alisema mnadhimu huyo wa Kambi ya Upinzani Bungeni.
Alisema
kinachofanywa na Rais Magufuli kilifanywa pia na watangulizi wake
waliounda tume kadhaa na kwamba mpaka azimio hilo linajadiliwa, bado
usafirishaji wa dhahabu inayochimbwa kwenye migodi mbalimbali nchini
unaendelea.
“Dhahabu
na madini mengine yanaendelea kusafirishwa hivi sasa. Ripoti za Profesa
Mruma na Profesa Osoro ni professorial rubbish. Ni uongo, uongo,
uongo,” alisema Lissu.
Ingawa
alitakiwa kufuta neno rubbish kwenye mchango wake, Lissu alifafanua
kwamba ripoti za wenyeviti hao wa kamati mbili za Rais za kuchunguza
makontena 277 ya mchanga wa dhahabu, hazina taarifa sahihi.
Kuhusu
azimio hilo kutokuwa na jipya, alisema Rais mstaafu, Benjamin Mkapa
aliunda kamati ya Jenerali (Robert) Mboma mwaka 2002, ya Dk (Jonas)
Kipokola mwaka 2004 kisha ya Dk (Enos) Bukuku mwaka 2005. Alisema hata
Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete naye aliunda mbili za Lawrence
Masha na Jaji Mark Bomani.
Alisema
kama Bunge linataka kupongeza kuhusiana na kamati zilizoundwa na Rais
Magufuli, basi halina budi kuanza na watangulizi hao ambao walifanya
kama anachokifanya sasa kwa masilahi ya Taifa huku akipendekeza semina
itolewe kwa wabunge ili kuwaongezea uelewa wa masuala ya madini na
kuwafanya wachangie wakiwa na ufahamu wa kutosha kuhusu sekta hiyo.
Lissu
alipingwa na Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde ambaye alitoa
sababu za kumpongeza Rais Magufuli akisema kuna tofauti kati ya kamati
alizoziunda na zile za watangulizi wake.
“Rais
ameenda mbali zaidi. Ripoti imepokewa hadharani na wananchi wote
wameisikia. Hii ni hatua ya mbele. Haiwezekani Taifa lisimpongeze Rais
anapofanya mambo yanayoonekana,” alisema.
Alisema
ameona clip (video fupi) za mawaziri wakuu wastaafu waliohamia
upinzani; Edward Lowassa na Frederick Sumaye wakimpongeza Rais kwa hatua
zake.
Lakini,
Mbunge wa Temeke (CUF), Abdallah Mtolea alionekana kuungana na Lissu
akiongeza kwamba maazimio hayo hayakuwa sawa kwa maelezo kwamba
kilichofanywa na Rais Magufuli mpaka sasa hakijapiga hatua kubwa zaidi
ya kilichofanywa na watangulizi wake.
Alisema
suala la msingi ni kudhibiti wizi wa rasilimali nchini akikumbusha
kwamba Kikwete pia aliunda tume lakini hata baada ya kupelekewa ripoti,
hakufanya chochote hatua ambayo Rais Magufuli amefikia mpaka sasa kwenye
vita aliyoianzisha.
Alisema
hoja ya wizi wa madini ilianzishwa siku nyingi na wabunge ambao
walionekana kuwa si wazalendo. “Kama Mkapa na Kikwete tungewapongeza kwa
kuunda tume leo ingekuwaje? Bunge tusiwe washangiliaji,” alisema.
Alikumbusha
pia kwamba Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CCM), Peter Serukamba alipiga
kelele, Dk Hamis Kigwangallah wa Nzega Vijijini (CCM) aliteswa, Tundu
Lissu, Zitto Kabwe wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo) na John Mnyika wa
Kibamba (Chadema) walilizungumza suala hilo lakini walibezwa.
Alisema kwa kuwa suala hilo sasa linazungumzwa na mtu anayependwa, linaungwa mkono.
Katika
mchango wake, Hasunga ambaye ndiye aliyekuwa mtoa hoja alisema hatua ya
Rais kuzuia usafirishaji wa mchanga nje ni muhimu inayopaswa kuungwa
mkono na Watanzania wote.
“Jimboni na mkoani kwangu kuna madini mengi, hatustahili kuwa maskini,” alisema.
Akiunga
mkono hoja hiyo, Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola alisema
anachokifanya Rais Magufuli ndicho alichoahidi hata kabla hajashika
wadhifa huo,
“Aliahidi
watu watalima kwa meno, tunaona mafisadi wakilima kwa meno. Namuomba
hata watu wanaowatetea wezi hawa awalimishe kwa meno pia.”
Mbunge
huyo ambaye aghalabu huzungumza kwa mbwembwe aliungwa mkono na Mbunge
wa Rufiji (CCM), Mohamed Mchengerwa ambaye alitaka neno uzalendo
liondolewe kwenye kamusi ya Kiswahili endapo kuna mtu atapinga
yanayofanywa na Rais Magufuli.
“Tunaamini mambo haya yakitekelezwa vyema tutakuwa na barabara za lami na hatutakuwa na deni la Taifa,” alisema Mchengerwa.