RAIS mstaafu ambaye pia ni Mdhamini wa Skauti Tanzania, Mzee Ali Hassan Mwinyi, Jumamosi (tarehe 18 Februari 2017) ameongoza matembezi ya hisani (Charity Walk) kwa ajili ya kuchangisha fedha za kufanikisha shughuli za Chama cha Skauti Tanzania kutoka kwa wadau na marafiki wa skauti kuelekea maadhimisho ya siku ya Skauti Afrika na miaka 100 ya Skauti Tanzania matukio yote mawili yanayotarajiwa kufanyika mwaka huu jijini Arusha.
Matembezi hayo ya hisani yameanzia
katika kiwanja cha Skauti kilichopo Upanga jijini Dar es Salaam na
kuishia katika bwalo la Maafisa wa Polisi (Police Officers Mess) la
Oysterbay kuanzia saa 12 asubuhi na kufikia tamati majira ya saa nne
asubuhi.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa
matembezi hayo, Skauti Mkuu wa Chama cha Skauti Tanzania, Mwantumu
Mahiza, alisema kuwa chama hicho kinatarajiwa kusherehekea Siku ya
Skauti Afrika na kuadhimisha miaka 100 tangu Skauti kuingia Tanzania
Bara (Tanganyika). Chama hicho hapa nchini kilianza mwaka 1917 na mwaka
huu wa 2017 kinatimiza miaka 100.
Uchangishaji mwingine wa fedha kwa njia
ya chakula (Dinner Gala Fund Raising) unategemea kufanyika Februari 24
katika Hoteli ya Serena ya ijini Dar es Salaam.
Skauti Mkuu wa Chama cha Skauti Tanzania, Mwantumu Mahiza, akizungumza jambo baada ya kuhitimisha matembezi. |
Kwa upande wake kamishna Mkuu wa Skauti
Abdulkarimu Shah amesema bado wanaendelea kuwahamasisha vijana kujiunga
katika chama hicho ili kuwa waadilifu, wajasiri, wabunifu na wenye
maarifa ili kufanikiwa na kuepukana na magonjwa yanayoepukika ikiwemo
Ukimwi.
Maadhimisho hayo yatafanyika juni 24
hadi julai mosi mwaka huu mjini Arusha, yenye kauli mbiu inayosema
“kuwajenga wazalendo na kufanya kazi kwa bidii kwa maendeleo ya nchi”.
Kamishna Mkuu wa Chama cha Skauti Tanzania, Abdulkarim Shaha, akizungumza jambo baada ya kuhitimisha matembezi. |
Aidha, Rais Mstaafu ALI HASSAN MWINYI,
amezindua mfuko wa kuchangia maandalizi ya mkutano wa Skauti wa Afrika,
uanaotarajiwa kufanyika Arusha, Machi mwaka huu ambapo ameonyesha
kufadhaishwa na baadhi ya wazazi wanaoshindwa kuwalea watoto wao katika
roho na kweli hivyo kujiingiza katika vitendo vya uvunjifu wa maadili na
kihalifu ikiwemo matumizi ya vileo na dawa za kulevya.
Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa
zaidi ya watu 5,000 kutoka nchi mbalimbali za Afrika na nje ya bara hilo
wanaotarajiwa kuhudhuria mkutano wa mwaka wa maskauti kuanzia Mach 8
mpaka 11 mwaka huu Mkoani Arusha, ikiwa ni maadhimisho ya kila mwaka ya
siku ya skauti Afrika yanayokwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 1OO
ya skauti Tanzania.
Mzee Mwinyi, ambaye ni Mwenyekiti wa
baraza la wadhamini wa skauti Tanzania, mwenye umri wa miaka 93 sasa,
akiwa bado ni mkakamavu na mwenye siha njema, alitembea kilometa 6.5
kutoka Makao makuu ya skauti Upanga mpaka viwanja vya bwalo la maafisa
Polisi Ostabei, katika matembezi ya hisani kuchangia maandalizi ya
mkutano huo unaotarajiwa kugharimu shilingi milioni 800.
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na mafunzo ya Ufundi, Profesa JOYCE
NDALICHAKO, ambaye kwa mujibu wa katiba ya skauti ni Rais wa skauti
kutokana na madaraka yake, amewasihi wazazi kuwapeleka watoto wao skauti
wakajifunze maarifa, stadi za maisha na uzalendo, badala ya kuwaacha
kama mifugo isiyo na mchungaji na katika hatua nyingine, amewaonya
walimu wote amabo shule zao zitabainika kuwa vijiwe vya wanafunzi
kujifunzia mambo yasiyofaa, serikali haitawavumilia.
Waziri wa Elimu, Sayansi,Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako, akizungumza jambo baada ya kuhitimisha matembezi. |
Habari na Sasi
Picha na Murtadhwa Elbahsan
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni