Na Veronica Simba – Dodoma
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesaini leseni za madini kutoka kwa wawekezaji mbalimbali waliowasilisha maombi na kutimiza taratibu zote zinazotakiwa kwa mujibu wa sheria.
Leseni ya kwanza iliyosainiwa ni ya uchimbaji wa kati wa dhahabu katika eneo la Masagalu, Handeni yenye namba ML 570/2016. Leseni hiyo imehamishwa kutoka kwa mmiliki wake wa awali ambaye ni Najim & Company Ltd kwenda kwa Shale Investments Tanzania Ltd.
Aidha, Waziri Muhongo alisaini leseni namba ML 572/2017 ya Sisti Mganga. Leseni hiyo ni ya uchimbaji wa kati wa madini ya ujenzi katika eneo la Itiso, Chamwino mkoani Dodoma.
Leseni nyingine iliyosainiwa na Waziri Muhongo ni ya
uchimbaji wa kati wa madini ya ujenzi aina ya kokoto, ambayo mmiliki
wake ni Said Abdallah. Leseni hiyo namba ML 573/2017 ipo eneo la
Chipite, Masasi.
Profesa Muhongo aliwataka waombaji na wamiliki wote
wa leseni za madini nchini, kuhakikisha wanatekeleza ipasavyo taratibu
zote kama zilivyobainishwa katika Sheria ya Madini ikiwemo ulipaji wa
mrabaha na kodi mbalimbali, kujenga mahusiano mema na jamii
zinazowazunguka pamoja na kuzingatia utunzaji na uhifadhi wa mazingira.
Zoezi hilo la utiaji saini lilifanyika hivi karibuni,
Makao Makuu ya Wizara mjini Dodoma na kushuhudiwa na wataalam
mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati na Madini.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
(kushoto), akisaini leseni za madini za wawekezaji mbalimbali
waliowasilisha maombi na kukamilisha taratibu zote zinazotakiwa.
Anayeshuhudia ni Mwanasheria wa Wizara, Khadija Ramadhan.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
(wa pili kutoka kulia), akikabidhi leseni iliyohamishwa kutoka kwa
mmiliki wake wa awali Najim & Company Ltd kwenda kwa Shale
Investment Tanzania Ltd.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
(wa pili kutoka kulia), akikabidhi leseni ya uchimbaji wa kati wa
madini ya ujenzi katika eneo la Itiso – Chamwino kwa mmiliki wake Sisti
Mganga. Kulia ni Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi Rayson Nkya.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
(wa tatu kutoka kushoto), akikabidhi leseni ya uchimbaji wa kati wa
madini ya ujenzi (kokoto) kwa mmiliki wake Said Abdallah iliyopo Chipite
wilayani Masasi. Wanaoshuhudia (kulia) ni wataalam kutoka wizarani.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
(katikati), akiwa katika kikao na wawekezaji mbalimbali wa madini
walioomba leseni (kushoto). Kulia ni wataalam kutoka wizarani.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
(kulia), akiwa katika kikao na wawekezaji mbalimbali wa madini
walioomba leseni (kushoto).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni