Na Frank Geofray-Jeshi la Polisi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mwigulu
Nchemba amewataka maofisa na askari Polisi kote nchini kuendelea kufanya
kazi kwa uadilifu ili kujenga taswira nzuri kwa wananchi wanaowahudumia
jambo ambalo litaongeza imani na ushirikiano katika kukomesha vitendo
vya uhalifu nchini.
Waziri Nchemba ameyasema hayo wakati alipokuwa
akifungua kikao kazi cha Maofisa wakuu wa Jeshi la Polisi kutoka makao
makuu, Makamanda wa Polisi wa Mikoa na vikosi kutoka bara na Zanzibar
kinachoendelea mkoani Dodoma.
Alisema Pamoja na Jeshi hilo kufanya kazi nzuri bado
linakabiliwa na changamoto ya baadhi ya askari na maofisa wasio
waadilifu wanaofanya vitendo vya kuwabambikia wananchi kesi na wakati
mwingine kuwabadilishia kesi ili kujenga mazingira ya kupatiwa rushwa
jambo ambalo ni kinyume na maadili ya askari Polisi.
“Fanyeni kazi kwa weledi hasa kwa kuwasimamia waliopo
chini yenu kwa kuwa wapo baadhi yao bado hawataki kubadilika na katika
awamu hii lengo letu ni kutoa haki kwa maskini hivyo ninyi kama
wasimamizi wa sheria mnapaswa kutenda haki mnapofanya kazi zenu na wale
wasiotaka kubadilika hamna budi kuchukua hatua ” Alisema Nchemba.
Aidha alilitaka Jeshi hilo kuwachukulia hatua
bodaboda wanaofanya makosa na wale wasiokuwa na makosa waachwe waendelee
na majukumu yao ya kujipatia kipato na kuachana na dhana ya kuwa kila
bodaboda ni mhalifu.
Kwa upande wake Inspekta Jenerali wa Polisi, IGP
Ernest Mangu alisema kikao hicho kinafanyika kwa siku tatu kwa lengo la
kufanya tathmini ya utendaji kazi kwa mwaka uliopita na kuweka mikakati
kwa mwaka huu ili kuendeleza juhudi za kukabiliana na vitendo vya
uhalifu hapa nchini.
Mangu alisema Jeshi hilo litaendelea na Oparesheni
zake za kupambana na uhalifu zikiwemo za dawa za kulevya, uhalifu wa
kutumia silaha na wizi wa mtandao kwa mikakati mipya ambayo itaibuliwa
katika kikao kazi hicho ili kuhakikisha hakuna mhalifu anayetamba hapa
nchini.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge mambo ya
nje na usalama Balozi Adadi Rajabu alisema kamati hiyo itaendelea
kuishawishi Serikali kuboresha maslahi na vitendea kazi vya Jeshi la
Polisi ili Jeshi hilo liweze kufanya kazi zake kwa ufanisi.
Ufunguzi wa Kikao kazi hicho ulihudhriwa pia na
Waziri Mkuu mstaafu Samweli Malechela, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan
Rugimbana pamoja na baadhi ya wabunge na Kamati ya ulinzi na usalama ya
mkoa wa Dodoma.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mwigulu
Nchemba (kulia) pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Ernest
Mangu wakiongozwa na askari wa kikosi cha bendera kuingia ukumbini kwa
ajili ya ufunguzi wa kikao kazi cha mwaka kinachowahusisha maafisa wakuu
wa jeshi la Polisi na makamanda wa mikoa na vikosi kinachofanyika
mkoani Dodoma. Picha na Hassan Mndeme-Jeshi la Polisi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mwigulu
Nchemba (kulia) akiongea na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Ernest
Mangu wakati wa hafla ya ufunguzi wa kikao kazi cha maafisa wakuu wa
jeshi la Polisi na makamanda wa mikoa na vikosi kinachofanyika mkoani
Dodoma. Picha na Hassan Mndeme-Jeshi la Polisi.
Baadhi ya maofisa wakuu wa Jeshi la Polisi wakiimba
wimbo wa maadili ya afisa wa polisi wakati wa hafla ya ufunguzi wa kikao
kazi cha maafisa hao na makamanda wa mikoa na vikosi kinachofanyika
mkoani Dodoma. Picha na Hassan Mndeme-Jeshi la Polisi. Picha Na Hassan
Mndeme.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni