Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam, Simon Sirro amesema kuwa tayari wameshapata taarifa za kupotea kwa Msanii wa Bongo Fleva hapa nchini, ‘Ibrahim Mussa’ maarufu kwa jina la Roma Mkatoliki na kuongeza kuwa tayari timu yake ya upelelezi imeshaanza kazi. |
Ameyasema hayo mapema hii leo wakati akizungumza na Katibu
wa Chama cha Wanamziki wa Kizazi Kipya Tanzania, Samweli Mbwana
alipotaka kujua kama Jeshi la Polisi lina taarifa ya kupotea kwa
mwanamziki huyo.
Sirro amesema kuwa taarifa za kupotea kwa msanii huyo
tayari wameshazipata na Jalada la upelelezi tayari limeshafunguliwa kwa
ajili ya upelelezi.
Ameongeza kuwa timu yake ya upelelezi iko mtaani kwa ajili
ya kujua kinachoendelea, na amewaomba wasanii na baadhi ya watu kutokuwa
wepesi wa kusambaza uvumi usiokuwa na ukweli ndani yake.
“Jamani mambo ya uvumi yaacheni, sio kitu kizuri
unamvumishia mtu kitu ambacho hakijui na wengine wanasema kuwa Serikali
inahusika kitu ambacho si cha kweli”,amesema Kamanda Sirro.
Aidha, Sirro amesema kuwa amepanga kukutana Waandishi wa
Habari Ofisini kwake ili kuweza kutoa ripoti kamili
kuhusu kupotea kwa msanii huyo wa Bongo fleva kwani timu ya upelelezi
tayari iko kazini.
Hata hivyo, amewatoa hofu wasanii na wananchi kwa ujumla
kwamba suala hilo linafanyiwa kazi, hivyo hakuna haja ya kuogopa na
kuendelea kuvumisha vitu visivyokuwa vya msingi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni