Dar es Salaam.
Rais John Magufuli amepokea kwa
mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za vifo vya Askari Polisi wanane
waliouawa kwa kushambuliwa na watu wenye silaha jana jioni katika eneo la
Jaribu Mpakani, Wilaya ya Kibiti Mkoani Pwani.
Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya
habari na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu leo inasema askari Polisi hao
walikuwa wakitoka kubadilishana doria wameshambuliwa kwa kupigwa risasi wakiwa
wanasafiri kwa gari katika barabara ya Dar es Salaam – Lindi.
Mkuu wa jeshi la polisi Tanzania IGP Ernest Mangu amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa taarifa zaidi zitatolewa na kamanda wa polisi mkoa wa Pwani. |
Taarifa zinasema kuwa polisi hao walikuwa
kwenye gari wakirejea kituoni kutoka kwenye doria na walishambuliwa na watu
waliotokea msituni.
Imeelezwa kuwa majambazi hao waliwavamia
ghafla polisi hao waliokuwa kwenye gari na kuwapiga risasi na kuwaua wote
palepale eneo la tukio, kisha kutokomea kusikojulikana na kwamba silaha zote
walizokuwa nazo (SMG) zilichukuliwa na watu hao.
Kutokana
na tukio hilo, Rais Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Jeshi la
Polisi nchini IGP-Ernest Mangu, familia za askari wote waliouawa, Askari Polisi
wote na Watanzania wote walioguswa na vifo hivyo.
Rais Magufuli amelaani
tukio hilo na matukio yote ya kuwashambulia askari polisi ambao wanafanya kazi
kubwa na muhimu ya kulinda raia na mali na ametaka Watanzania wote watoe
ushirikiano katika kukomesha vitendo hivyo
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni