Bodi ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) imekutana jijini
Dar es Salaam leo Machi 30, 2017. Pamoja na mambo mengine imejadili
mwenendo wa vyombo vya habari ndani ya wiki moja tangu tulipotoa msimamo
wa kutotangaza habari za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Bodi imepitia habari za Mkuu wa Mkoa zilizochapishwa tangu
ulipotolewa msimamo wa kumfungia. Bodi inapenda kawapongeza wahariri
wote waliotekeleza kwa usahihi msimamo wa kutochapisha habari za Mkuu wa
Mkoa kwa wiki nzima.
Bodi inapenda kusisitiza kuwa wahariri katika vyombo vya
habari; magazeti, radio na televisheni waendelee na msimamo wa kususia
habari za Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda, hadi atakapotimiza takwa la kuomba
radhi kwa tukio la kuvamia kituo cha Clouds.
Aidha, Bodi inatoa wito kwa viongozi wa mitandao ya kijamii
kuunga msimamo huu. Bodi inapenda kufafanua kuwa Mhe. Makonda amewekewa
vikwazo Maalum (Smart Sanction) kwa mikutano atakayoiandaa au matukio
atakayoyaongoza habari zake hatutazichapisha.
Wakati huo huo, kituo cha Clouds kimepongezwa kwa
kumsimamisha kazi mtangazaji aliyekiuka msimamo wa kutotangaza habari za
Makonda.
Bodi pia imewasiliana na Uongozi wa UTPC na kukubaliana kwamba msimamo huu uendelee.
Theophil Makunga,
Mwenyekiti TEF
Imetolewa Leo,
Machi 30, 2017