Chama Cha Mawakili (Tanganyika Law Society-TLS), kimepokea kwa mshtuko
na masikitiko mkubwa taarifa za mauaji ya askari wetu wa jeshi polisi
nane katika eneo la Jaribu Mpakani wilaya ya Kibiti. Vijana wetu hao
wameuawa wakitekeleza majukumu yao ya kulitumikia taifa letu na kikundi
cha watu wasioitakia mema nchi yetu na wakaamua kuchukua maisha yao
kikatili na katika utaratibu wa ajabu ambao hauwezi kukubalika kwa
maelezo ya aina yoyote ile.
Tunatoa salamu zetu za rambirambi kwa wananchi wa mkoa wa
pwani na watanzania kwa ujumla, Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest
Mangu, pia tunatoa pole kwa familia za wapendwa hawa , jamaa zao,
marafiki na watumishi wenzao wa jeshi la polisi. Sisi kama Chama cha
mawakili tunalaani vikali tukio hili la mauaji ya askari na matukio
Mengine yanayoshabihiana na tukio hili la Kibiti.
Hata hivyo tunaiomba serikali kupitia jeshi la polisi na
vyombo vingine vya dola kufanya uchunguzi wa kina juu ya mauaji haya
yakiunganishwa na mlolongo wa matukio mengine mengi yanayotokea huko
mkoani pwani na nchini kwa ujumla hasa yale yanayohusu mauaji ya raia
wakiwemo viongozi wa vitongoji na serikali za kijiji, mauaji ya mara kwa
mara ya askari na makamanda wetu ambayo yameonekana kukithiri katika
kipindi cha takriban mwaka mmoja sasa pamoja na unyang'anyi wa silaha.
Chama cha mawakili kinaamini matukio kama haya yumkini ni
matokeo ya matukio mengine ya mauaji, ujambazi, uporaji na au utekaji wa
raia yaliyopata kutokea lakini vyombo vyetu vya dola vikaonekana
kutokuchukua hatua madhubuti ya kuhakikisha wahalifu husika wanatiwa
nguvuni na kupelekwa mahakamani.
Wito wetu ni kuwaomba wananchi kutulia, kutoa ushirikiano
kwa jeshi letu la polisi na vyombo vyote vinavyohusika na ulinzi na
Amani wa nchi yetu, hasa katika kipindi kama hiki ambacho ulinzi na
usalama wa raia unaingia katika majaribio ya hali ya juu, ndio kipindi
cha kushikamana na kuhakikisha matendo ya namna hii yanakomeshwa mara
moja.
Mwisho tunamwombea kijana wetu aliyejeruhiwa katika tukio
hili apone haraka na arudi kwenye majukumu yake kama kawaida ya kujenga
taifa, pia tunaungana na familia za marehemu, jeshi la polisi kuwaombea
dua waliouwawa ili wakapumzike kwa Amani, na Mwenyezi Mungu Azilaze Roho
zao Mahala Pema Peponi. AMINA
Imetolewa na Rais wa Chama-Tundu A. Lissu
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni