Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia
Suluhu Hassan amewahimiza wananchi kudumisha na kuuenzi Muungano wa
Taganyika na Zanzibar na kuwahakikishia wananchi wa pande Mbili kuwa
kero chache za Muungano ambazo zimebaki zitamalizwa kwa mazungumzo kama
hatua ya kudumisha Muungano huo.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo
kwa nyakati tofauti katika Mahojiano na vyombo Mbalimbali vya habari
katika kuelekea katika Kilele cha Maadhimisho ya Muungano wa Tanganyika
na Zanzibar ambapo sherehe za kitaifa mwaka huu kwa mara ya Kwanza
zitafanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri Mjini Dodoma.
Makamu wa Rais amesisitiza kuwa tangu Muungano huo uasisiwe
umekuwa na manufaa makubwa kwa pande zote Mbili kwani jamii
zimefahamiani na kushirikiano vizuri katika shughuli za kiuchumi na za
kimaendeleo hasa uimarishaji wa ulinzi na usalama kwa wananchi wa pande
Mbili.
Aidha,Amesema hatua zinazochukuliwa za kutatua kero za
Muungano kwa haraka ni jambo jema na la msingi kwani linalenga
kuhakikisha Muungano ambao umefikisha miaka 53 sasa unakuwa ni Muungano
wa mfano wa kuigwa Duniani.
Kuhusu elimu ya Muungano wa Vijana, Makamu wa Rais Mhe
Samia Suluhu Hassan amesema upo umuhimu mkubwa kwa taasisi za Kiserikali
za pande Mbili kuweka mikakati mizuri ya kuelemisha vijana wa sasa
kujua umuhimu wa Muungano ili waweze kuuelewa na kuudumisha.
Amesema kwa sasa vijana wengi wanafuatilia sana mitandao ya
kijamii hivyo ni muhimu kwa taasisi za kiserikali zinazoshughulia
Muungano kuweka utaratibu wa kupeleka ujumbe mbalimbali kuhusu Muungano
kwa jamii hasa vijana kwa ajili ya kuwaelimisha faida za Muungano.
Makamu wa Rais pia amehimiza makundi mbalimbali ya kijamii
wakiwemo viongozi wastaafu nchini waendelee na jitihada zao katika
kuelimisha umma ili kuuelewa vizuri Muungano kwa ajili ya faida ya jamii
nzima na ya Taifa kwa ujumla.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
DODOMA.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni