Serikali imeendelea kuchukua hatua kwa kuendelea kutoa
elimu katika Halmashauri za Wilaya, Manispaa na Miji 72 ili kuondokana
na tatizo la ndoa za utotoni zinazobababisha watoto kukosa haki ya
msingi ya kupata elimu.
Akijibu swali la Mhe. Anna Kilango Malecela Mbunge wa Viti
Maalum (CCM) lililouliza Je, Serikali ina Mkakati gani wa kutokomeza
ndoa za utotoni? Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsi Wazee na
Watoto, Dk. Hamisi Kigwangalla amesema kuwa msisitizo utazidi kuwekwa
katika utoaji wa elimu kwa familia, wazee wa mila na jamii kwa ujumla.
“Tutajikita kutoa elimu zaidi ili jamii iachane na mila na tamaduni zilizopitwa na wakati za kuoza watoto wa kike,” alisisitiza Dkt. Kigwangalla.
Ameongeza kuwa Serikali inatambua athari kubwa
zinazosababishwa na ndoa za utotoni katika jamii ya watanzania na
itaongeza nguvu katika kutoa elimu na kupambana na wale wote
watakaojihusisha kwa namna moja au nyingine kuwanyima watoto wa kike
haki yao ya kupata elimu.
Aidha kulingana na takwimu za Afya na Idadi ya Watu nchini
za mwaka 2016 ndoa za utotoni zimeshamiri katika mikoa ya Shinyanga kwa
asilimia 59, Tabora kwa asilimia 58, Mara kwa asilimia 55 na Dodoma kwa
asilimia 51 hivyo Serikali itaendelea kupambana kutokomeza ndoa za
utotoni nchini.
Kwa upande wa muundo wa kisera na kisheria, Serikali
imezifanyia maboresho Sera na Sheria ili kumlinda mtoto wa kike dhidi ya
ndoa na mimba za utotoni pamoja na marekebisho ya Sheria ya Elimu Sura
353 ambayo inatoa adhabu ya kifungo kisichopungua miaka 30 kwa mtu
yoyote atakayempa mimba mwananfunzi wa shule ya Msingi au Sekondari.
Katika kutokomeza ndoa na mimba za utotoni Serikali itaanza
utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza Ukatili dhidi ya
wanawake na watoto mwezi June 2017 unaojumuisha Sekta zote zinazohusu
wanawake na watoto kwa lengo la kutokomeza aina zote za ukatili na
kupunguza mimba za utotoni kutoka asilimia 47 hadi 10 ifikapo mwaka
2020.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni