Na Regina Mkonde
Rais
John Magufuli Jumamosi ya Mei 20, 2017 katika mkutano wa 18 wa Wakuu wa
Nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)anatarajiwa
kumkabidhi kijiti cha uenyekiti wa jumuiya hiyo Rais wa Uganda, Yoweli
Museveni baada ya Tanzania kuingoza EAC kwa vipindi viwili mfululizo.
Hayo
yamesemwa jana Mei, 18 na Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Augustine
Mahiga katika Mkutano wa 34 wa Baraza la Mawaziri la EAC, ambapo
alieleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi ambacho Tanzania
iliiongoza jumuiya hiyo, ikiwemo kuridhia maombi ya muda mrefu ya
uanachama, ya nchi ya Jamhuri ya Sudan Kusini na kuipatia uanachama
kamili wa jumuiya hiyo.
“Tanzania
tumemaliza muda wetu baada ya kuiongoza vipindi viwili mfululizo, Rais
Magufuli Jumamosi atamkabidhi uenyekiti Rais Museveni wa Uganda,”
alisema.
Alieleza
kuwa, pamoja na Rais Magufuli kukabidhi kijiti hicho kwa Museveni, Rais
Mstaafu Benjamin Mkapa anatarajiwa pia katika mkutano huo kuwasilisha
ripoti ya mazungumzo ya pamoja ya kuleta amani, ikiwa ni utekelezaji wa
agizo la wakuu wa nchi wa EAC lililotolewa mwezi Januari,2017.
Kuhusu
mkutano wa Baraza la Mawaziri wa EAC uliofanyika jana Mei 18, 2017,
alisema wajumbe wa baraza hilo watajadili ushirikiano wa masuala
mbalimbali yanayohusu jumuiya hiyo, ikiwemo ushirikiano kibiashara,
uwekezaji, elimu pamoja na huduma mbalimbali za kuendesha nchi wanachama
hasa ujenzi wa miundombinu na uchukuzi.
“Kwanza
Tanzania itatoa ripoti ya ushirikiano kwa kipindi cha miaka miwili
iliyoiongoza EAC ikiwemo ya ushirikiano kibiashara, kielimu na huduma za
kuendesha nchi,” alisema.
Alisema
wajumbe hao watajadili namna ya kuondoa na au kupunguza vikwazo visivyo
vya kisheria hasa vinavyokwamisha biashara ikiwemo ushuru wa forodha,
vizuizi vya magari, aina za biashara, na kwamba watajadili namna ya
kuanzisha soko imara la pamoja.
“Kuna
vikwazo visivyo vya lazima vinavyokwamisha biashara kwa nchi
wananchama, mfano Tanzania tuna vyombo viwili vinavyopima ubora wa
bidhaa, TBS na TFDA ambapo wenzetu wanasema ngazi hizi mbili zinazuia
biashara zao, kwa hiyo tutazungumzia suala hili. Pia tutajadili namna ya
kutekeleza lengo letu la kuzuia uingizwaji wa nguo za mitumba kutoka
nchi za nje ya jumuiya hii,” alisema.
Kwa
upande wa elimu, Balozi Mahiga alisema wajumbe hao watajadili namna ya
kuanzisha mfumo wa elimu ambao utasaidia kuondoa tofauti ya upatikanaji
elimu katika vyuo vya EAC ikiwemo wanafunzi wa jumuiya hiyo kupata elimu
kwa malipo na vigezo vinavyo fanana na kwamba kusiwepo na vikwazo.
“Tulikuwa
na chuo kimoja tu cha jumuiya, lakini sasa tuna vyuo tanzu katika nchi
ya Tanzania, Kenya na Uganda kwa hiyo kuna umuhimu wa kuwa na mfumo wa
elimu kwa wanafunzi kupata elimu kwa malipo na vigezo vinavyofanana.
Mwanafunzi wa Tanzania akienda Kenya asome kwa vigezo na gharama ileile
anayolipa mwanafunzi wa Kenya,” alisema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni