Na Benny Mwaipaja, WFM-Dodoma
Serikali
imeeleza kuwa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haijawahi kumuhusisha Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika
ukaguzi wa Balozi au ukaguzi wowote ule kama Umoja wa Mataifa kwa sababu
hakuna ulazima wa kufanya hivyo Kikatiba na Kisheria.
Hayo
yameelezwa Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango
(MB), Dkt. Ashatu Kijaji, alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa
Kiwengwa Khamisi Mtwana Ally (CCM), aliyetaka kujua ni mara ngapi Ofisi
hiyo ya Bara imeishirikisha Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali ya Zanzibar.
Akijibu
swali hilo Dkt. Kijaji alisema kuwa, Ofisi hizo kila moja ina mipaka
yake ya kufanya ukaguzi na kwamba jukumu la ukaguzi wa Taasisi za
Muungano lipo kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Ofisi
ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali imeanzishwa kwa mujibu wa
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na kwamba
majukumu ya Ofisi hiyo yameainishwa katika ibara ya 143(2) ya katiba
hiyo”. Alisema Dkt. Kijaji
Dkt
Kijaji aliongeza kuwa, eneo hilo linamtaka Mdhibiti na Makguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali kufanya ukaguzi angalau mara moja kila mwaka na kutoa
taarifa kuhusu ukaguzi wa Hesabu za Serikali, Bunge na Mahakama.
Aidha,
Dkt. Kijaji alisema kuwa majukumu hayo yameainishwa katika kifungu cha
10 cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma ya mwaka 2008 na kanuni zake za mwaka
2009.
Dkt.
Kijaji alifafanua kuwa, ukaguzi wa Balozi unafanyika chini ya fungu 34,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kuwa
Ofisi zote za Ubalozi ni sehemu ya fungu 34.
“Hivyo
basi, ukaguzi wa Balozi kama ilivyo kwa Taasisi nyingine za Muungano
unafanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania .”alisema Dkt. Kijaji
Aliongeza
kuwa, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Zanzibar,
majukumu yake yameainishwa kwenye ibara ya 112 ya Katiba (3) ya katiba
ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Akiongeza
majibu ya swali hilo, Waziri wa Mazingira na Muungano, Januari Makamba
alisema kuwa wakaguzi wa pande zote kutoka Tanzania Bara na Visiwani
hufanya kazi kwa kushirikiana katika mambo ya ukaguzi wa hesabu za
serikali.
Katika
swali la nyongeza Mbunge wa Mkwajuni, Ally Zubeir Ngwali (CUF), alihoji
ni kwanini fedha za mfuko wa Jimbo hazijawahi kukaguliwa na
zitakaguliwa kwa utaratibu upi.
Akijibu
swali hilo, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jaffo alisema upo utaratibu maalum wa
kushughulikia mambo hayo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni