WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amenunua hisa za kampuni ya Vodacom Tanzania Plc
zenye thamani ya sh. milioni 10 pamoja na nyingine za sh. milioni 10 kwa
ajili ya mke wake, Mary Majaliwa.
Waziri
Mkuu amechukua hatua hiyo Ijumaa, Mei 5, 2017 wakati akizungumza na
waandishi wa habari mbele ya wakuu wa Masoko ya Hisa na Dhamana; Soko la
Hisa la Dar es Salaam, viongozi wa Baraza la Uwezeshaji na kampuni ya
Vodacom katika ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es
Salaam.
Waziri
Mkuu amewasihi Watanzania walioko ndani na nje ya nchi wachangamkie
fursa ya kununua hisa hizo ili waweze kuwa wamiliki wa kampuni kupitia
hisa zao. “Hii ni fursa kwa Watanzania kumiliki kampuni. Ukinunua hisa,
unashiriki kikamilifu kumiliki kampuni na pia unaboresha uchumi wako
binafsi. Ninawasihi Watanzania wote tumieni fursa hii kununua hisa hizo
kabla muda haujaisha,” alisisitiza.
Alisema
watumishi wa umma wamepewa ya kununua hisa hizo kupitia mipango
iliyowekwa na Makatibu Wakuu wao lakini pia amewasihi viongozi
mbalimbali wa Serikali na taasisi wachangamkie fursa hiyo ili nchi iweze
kupata kodi kupitia makampuni hayo.
“Hii
ni fursa kwa kila Mtanzania, kwa viongozi kwa taasisi na mashirika ya
umma, taasisi binafsi, wajasiriamali wadogo kama akinamama lishe au
madereva wa bodaboda. Watanzania walioko nje ya nchi (Diaspora) nao pia
wanunue hisa kwani watakuwa wanachangia uchumi wa nchi na wakati huo
wanaweka akiba nyumbani,” aliongeza.
Akimkaribisha
Waziri Mkuu kuzungumza na hadhira hiyo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk.
Philip Mpango uwekezaji kwenye hisa ni njia mojawapo ya kuwawezesha
Watanzania kumiliki uchumi wa nchi.
“Huko
mtaani ukisema uchumi wa nchi unakua, watu wanabisha wakidai kuwa
hawaoni unakua kwa sababu hawana fedha mifukoni. Hii ni fursa nyingine
ya kuwawezesha kukua kiuchumi, ninaomba waichangamkie,” alisema.
Alisema
sekta ya mawasiliano ni miongoni mwa sekta inayokua kwa kasi hapa
nchini kwani katika robo tatu ya mwaka, sekta hiyo imekua kwa asilimia
11.3. “Niwasihi Watanzania wenzangu, tununue hisa za Vodacom ili tuweze
kuboresha uchumi wetu,” alisema.
Alisema
anatoa ombi maalum kwa wafugaji kukubali kuuza mifugo yao na kununua
hisa ili kupunguza idadi ya mifugo yao, jambo ambalo alisema litapunguza
migogoro baina yao na wakulima.
“Wakulima
wa vitunguu, alizeti, maua au wafugaji wa samaki nao pia wanaweza
kununua hisa na kuwa na mitaji kwa ajili ya shughuli zao. Ninawasihi
wote watumie fursa hii ili kumiliki kampuni,” alisema.
Kwa
upande wake, Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Soko la Mitaji na Dhamana, Bi.
Nassama Masinda alisema amefurahishwa kuona Waziri Mkuu akinunua hisa
za kampuni ya Vodacom katika soko la awali.
Alisema
uuzwaji wa hisa hizo ni utekelezaji wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2016
kwa lengo la kuwawezesha Watanzania kuwa wamiliki wa makampuni ya simu
za mikononi hapa nchini. “Marekebisho ya Sheria ya Mawasiliano ya
Kielektroniki na Posta sura ya 306 yanazitaka kampuni za simu na
mawasiliano ya kielektroniki kuuza si chini ya asilimia 25 ya hisa zao
kwa umma wa Tanzania kupitia masoko ya mitaji (IPO).”
Alisema
baada ya hapo hisa hizo zinapaswa kuorodheshwa kwenye soko la Hisa la
Dar es Salaam baada ya kukidhi matakwa ya Sheria ya Masoko ya Mitaji na
Dhamana, sura ya 79. Kampuni ya Vodacom ilitoa hisa milioni 560 kwa umma
kwa bei ya sh. 850 kila moja na hivyo kutarajia kukusanya sh. bilioni
476.
Alisema
hivi sasa, wawekezaji kwenye masoko ya mitaji ni watu 500,000 tu
ikilinganishwa na Kenya ambayo ina wawekezaji milioni 1.7; Uganda
(40,000) na Rwanda (14,000). “Vodacom ina wateja milioni 6.2, iwapo nusu
ya wateja wake wote watashiriki ununuzi wa hisa, idadi ya wawekezaji
kupitia masoko ya mitaji na dhamana itaongezeka kwa asilimia 1,140. Na
haya yatakuwa ni mageuzi makubwa katika sekta ya masoko ya mitaji si
hapa nchini tu bali katika Afrika Mashariki,” alisema.
Mtendaji
Mkuu wa Dodacom, Bw. Ian Ferrao alisema mauzo ya hisa yanayofanywa na
kampuni hiyo ni makubwa mara nne ya mauzo ambayo yamewahi kufanyika hapa
nchini.
Alisema
kampuni hiyo ambayo imekwishafanya kazi kwa miaka 17 hapa nchini,
imewekeza zaidi ya sh. trilioni mbili katika mtandao wa mawasiliano
nchini Tanzania.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, MEI 5, 2017.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni