Serikali
imesema imebadili utaratibu gerezani kwa watu watakaotumikia kifungo
cha miaka 30 jela kutokana na kuwapa mimba au kuoa mwanafunzi.
Utaratibu
huo uliobadilishwa ni wa kuhesabu siku, ambapo sasa mfungwa wa makosa
hayo atahesabiwa usiku na mchana kuwa ni siku moja badala ya usiku na
mchana kuwa siku mbili ilivyo kwa wafungwa wengine.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa ndiye aliyefichua suala hilo jijini hapa jana,
alipozindua Kampeni ya Siku 16 Kupinga Ukatili wa Kijinsia ambayo
hufanyika kila mwaka kuanzia Novemba 25 hadi Desemba 10.
Kampeni
hiyo imeratibiwa na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo
Barani Afrika (WiLDAF) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa
maendeleo.
Akizungumza
na wananchi katika uzinduzi huo, Majaliwa alisema serikali imewezesha
marekebisho ya Sheria ya Elimu na kulifanya kosa la kumpa mimba kuoa au
kuolewa mwanafunzi kuwa kosa la jinai na pale inapothibitika, adhabu
yake ni kifungo cha miaka 30, hivyo watakaokutwa na mkono wa sheria
"watakiona cha mtema kuni".
“Huwa
nalizungumza hili, mtu yeyote atakayekutwa na tukamkamata amempa mimba,
amemuoa, amemchumbia mwanafunzi, adhabu yake ni kubwa sana na kabla
hujafanya tendo hilo jiulize una miaka mingapi ili ujue utakapoadhibiwa
ukajumlisha na miaka yako tuone ukienda gerezani ujue unatoka na miaka
mingapi," Majaliwa alisema na kuongeza:
"Kule
gerezani tumesema utaratibu wa kuhesabu mchana na usiku kuwa ni siku
mbili, kwenye adhabu hii ni siku moja tu, kama ni miaka 30 basi miaka 30
kweli, sasa je, miaka 30 utarudi ukiwa hai wewe?"
Waziri
Mkuu aliwataka Watanzania kuwa macho na wale wote wasiowatakia mema
wanafunzi, akiagiza kuwa "mtu akikutwa amesimama kwenye kona
isiyoeleweka na mwanafunzi ashughulikiwe."
“Na
wale wataalamu wa kuwasalimia wanafunzi mara nne nne kwa siku, ole wako
tukikukamata utakiona cha mtema kuni, kwa hiyo eneo hili tumeimarisha
kumlinda mtoto wa kike na serikali ya awamu ya tano imewekeza kwa mtoto
wa kike," alisema.
Alisema
mpango wa kufikia asilimia 50 kwa 50 utafikiwa kama ikiwekezwa kwa
mtoto wa kike na serikali imedhamiria kufikia hatua hiyo.
Majaliwa
alisema ukatili wa kijinsia hususan dhidi ya wanawake na watoto
unarudisha nyuma juhudi za serikali za kuhakikisha kuwa mapinduzi ya
viwanda na kilimo yanafikiwa.
“Hatuwezi
kuwa na taifa linalozalisha na kufikia malengo ya kuwa nchi ya uchumi
wa kati iwapo muda mwingi unatumika kuamua migogoro na kuhudumia
waathirika wa ukatili wa kijinsia badala ya kushiriki katika shughuli za
uzalishaji,” alisema.
Aliwaagiza
wakuu wa mikoa kuhakikisha wanasimamia uanzishwaji wa kamati za ulinzi
wa wanawake na watoto kwenye mikoa, halmashauri, kata na vijiji kama
ilivyoelekezwa kwenye mwongozo wa uratibu wa mpango wa taifa wa
kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
“Nawaagiza
wakurugenzi wa halmashauri zote kuanzisha programu za kijamii za
kutokomeza ukatili wa kijinsia katika halmashuari husika
zitakazozingatia hali halisi na kuzitengea bajeti programu hizo,"
alisema.
Majaliwa
pia aliwataka wadau kutumia siku hizo kuwasilisha mapendekezo kama kuna
upungufu unaohitaji sheria zitungwe kuwasilisha kwa Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa ajili ya kutunga sheria.
Waziri Mkuu pia alisema kumekuwa na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yanayoleta madhara kwa jamii.
Aliagiza
kila taasisi na kampuni ya simu kuhakikisha inawachukulia hatua kali
dhidi ya watakaobainika wanatumia vibaya mitandao ambayo inarudisha
nyuma jitihada za kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
“TCRA
(Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano) ambao ndiyo wanaofuatilia
watumiaji wote wa mitandao, hakikisheni mnadhibiti na wale wote
mnaojidanganya kuwa kuna mitandao haionyeshi, tukikukamata ndio utajua
kuwa tunakuona," alisema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni