
Mbunge wa Jimbo la Mtama mkoani Mtwara kupitia tiketi ya
CCM, Mhe. Nape Nnauye amtaka Rais Magufuli aunde tume huru ambayo
itaweza kuchunguza matukio ya uhalifu ya uvamizi wa studio unaoendelea
nchini.
Hatua hiyo inatokana na matukio ya kiuhalifu yanayoendelea
Tanzania na kuacha maswali mengi vichwani mwa wananchi kushindwa
kufahamu kuwa watu hao na vikundi hivyo vya kihuni vinavyofanya vitendo
hivyo vinapata wapi mamlaka hayo kuwa na nguvu kushinda Dola.
“Ombi langu kwa Rais namuomba aunde tume huru ichunguze
matendo haya yasijirudie tena kwa sababu yasipochukuliwa hatua
yataharibu sura ya Tanzania pia yataweza kuibuka makundi ya wahuni
kuanza kuteka watu nao kwa kuwa hakuna hatua zinazochukuliwa. Tumsaidie
Rais Magufuli kwa kumwambia ukweli naimani atasikia na atafanyia kazi
kwa kuwa Rais wetu anapenda kusikiliza watu”. Alisema Nape
Aidha Mbunge huyo amesema watu wanaofanya mambo hayo
wanalengo la kuwagombanisha wananchi na Rais wao jambo ambalo sio zuri
kwa taifa.
"Juzi amepotea msanii Roma Mkatoliki na wengine lakini
mpaka sasa haifahamiki wapo wapi, yaani kama vile amepotea Nzi,
tulisikia kijana mmoja wa CHADEMA anaitwa Ben Sanane amepotea saizi
miezi mitano imepita, matendo haya ya kina Ben Sanane, Roma Mkatoliki,
na wengine yanajenga chuki ya wananchi kwa Rais, lakini pia yanajenga
chuki kwa wananchi na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ". Alisema Nape Nnauye
Vile vile Nape amesema yeye mpaka sasa haamini yule mtu
aliyemtolea silaha siku ya mkutano wake na wanahabari kama alitumwa ila
shida aliyokuwa nayo ni kutaka kujua vyombo vya ulinzi na usalama
vinafanya nini mpaka matukio yote yanatokea.
![]() |
| Nape akilia kwa simanzi alipokuwa akilakiwa na akina mama waliolala chini iliatembee juu yao |
![]() |
| Nape akisalimiana na wapiga kura wake |
==> Haya ni Maneno ya Nape
Nilipopewa Uwaziri kwa miezi 15, sina mashaka, nilifanya kazi kwa umakini mkubwa kwa kutumia uwezo wangu wote. Kama ambavyo siku ya kuteuliwa hatukujadiliana, miezi 15 ilipopita aliyeniteua aliamua kufanya mabadiliko ya baraza.
Kama ikibainika kuwa alivamia kituo cha Clouds, alafu nisipochukua hatua, sitakuwa na sababu ya kuendelea kuwa waziri. Nilipogundua ni kweli alivamia Clouds, niliamua kuchukua hatua na kusimamia maneno yangu nisionekane mpumbavu ni mimi.
Nilipotishiwa kwa bastola, nilimwambia yule mtu taratibu, unaharibu sababu tukio lile lilikuwa likirushwa mubashara. Yule aliyenitisha walisema si Polisi, mara hajulikani.Lakini mtu mwingine akinyanyua bastola hapa, Polisi hawatakuacha. RPC alikuwa pale, kama hakuwa Polisi kwanini wasimkamate? Na mtu yule si kweli kwamba hajulikani, anajulikana.
Mazingira ya kupotea kwa Ben Saanane yanautata mkubwa sana. Watu wengi sana wanatishiwa sasa. Juzi studio wametekwa wanne. Matukio yanayoendelea sasa nchini yanawafanya watu kuwa na hofu. Hawaamini kama wakitoka watarudi majumbani mwao salama. Namuomba Rais wangu aunde tume huru ya kuchunguza matendo haya ili impelekee taarifa kamili aweze kuchukua hatua.
Tusipochukua hatua, yatajitokeza makundi ya wahuni nao watapitia mlango huo huo kwa sababu hakuna hatua zinazochukuliwa. Matendo haya yasipokomeshwa haraka, CCM tutapata tabu sana kwenye uchaguzi wa mwaka 2020.


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni