
SERIKALI inakusudia kuajiri watumishi wapya wa umma 52,436
katika mwaka ujao wa fedha. Aidha, madaktari wapya 258 waliokuwa waende
kufanya kazi nchini Kenya, lakini wakakwama kutokana na kuwekewa
pingamizi la kimahakama na wenzao wao huko na hivyo Rais, Dk John
Magufuli kuamuru waajiriwe mara moja nchini, watarajiwa kuanza kazi
keshokutwa Jumatatu.
Hayo yalisemwa bungeni juzi usiku na Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais anayeshughulikia Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Angellah Kairuki alipokuwa anatoa ufafanuzi wa lini Serikali
itaendelea kuajiri watumishi wa kada nyingine, kama ilivyoulizwa na
Mbunge wa Viti Maalumu, Anna Lupembe (CCM).
“Azma ya serikali, kwanza kabisa hatuwezi kuajiri wananchi
wote, tumekuwa tukisikia hapa wahitimu hawana ajira, wengine wanaendesha
bodaboda… tunapopanga idadi ya watumishi wa kuajiriwa, tunaangalia
mambo mengi, kuanzia mahitaji, vipaumbele hadi uwezo wa kibajeti.
“Tayari tumeshaanza kutoa vibali vya ajira zaidi ya watu
9,700 na tutaendelea kufanya hivyo, na hivi karibuni Rais amebariki
kuajiriwa kwa madaktari wapya 258 na Jumatatu (keshokutwa) wanaripoti
kazini.
Tutaendelea kuajiri na wataalamu wa kada nyingine, kabla ya
kumalizika kwa mwaka huu wa fedha mwezi Juni tutakuwa tumejiajiri kwa
idadi tutakayoipanga kwa awamu, na katika mwaka ujao wa fedha
tutaendelea kuajiri watumishi wengine wa umma zaidi ya 52,436,” alisema.
Hata hivyo, alisisitiza Serikali itahakikisha hairudii
makosa ya kuajiri watumishi hewa, wasio na sifa na weledi unaohitajika.
Alisema kwa kiasi kikubwa uhakiki wa watumishi wa umma kwa ujumla
umekwisha, lakini kazi hiyo ni endelevu, kwani serikali itaendelea
kufanya hivyo mara kwa mara.
Alisema matunda ya uhakiki wa watumishi wa umma umebaini
watumishi hewa 19,708 na ambao wameshaondolewa katika orodha ya
mishahara ya watumishi wa umma. “Hawa wangeachwa, Serikali ingekuwa
inapoteza kiasi cha Sh bilioni 19.8 kila mwezi, lakini fedha hizi
zimeokolewa kupitia uhakiki wa watumishi wa umma.
Tunafanya haya kwa nia njema. Mathalani tusingewatoa hawa,
si wangeziba nafasi za ajira za wengine na fedha ngapi zingepotea?”
alihoji. Alisisitiza kuwa, wizara hiyo itaendelea kutimiza majukumu yake
kwa vitendo ili kurejesha nidhamu ya serikali na utumishi wa umma kwa
kuongeza uwazi na kusimamia sheria, kanuni na taratibu za uwajibikaji wa
viongozi wa watumishi wa umma ili wawajibike kwa wananchi ambao ndio
wateja na waajiri wakuu wa watumishi wa umma.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene, akijibu hoja za
wabunge, hasa la uhamisho wa watumishi wakiwemo wanandoa
wanaotenganishwa, alikemea tabia ya maofisa watumishi kuzuia wenye ndoa
kuhama kutoka kituo kimoja cha kazi kwa lengo la kuwafuata wenzao.
Alisema kuwazuia ni kuwanyima haki ya msingi, na kuwaagiza
wabunge katika maeneo yao wasaidia kusimamia haki za watumishi. Lazima
sheria za utumishi zizingatiwe, walimu hawa au watumishi wanayo haki ya
kutoka sehemu moja kwenda nyingine, lakini pia kuishi na wenza wao,
lakini utadhani mtumishi anapoomba ni kama anasaidiwa, hapana ni haki
yake ya msingi, waheshimiwa tusimamie haki za watumishi,” alisema
Simbachawene
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni