Powered by: Elbahsan Web & Blog Designer
Do want your Network!!! Website or Blog-Spot, Try Us: Elbahsan Web & Blog Designer Contact Us Now... Calll; +255743550360 | +255788680558 Email; murtadhaalbahsan@gmail.com

Zawamba Photo Production

Ijumaa, 26 Mei 2017

MIAKA MIA MOJA YA SKAUTI TZ: VIONGOZI WA CHAMA CHA SKAUTI WAKUTANA NA MAKAMO WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR

Chama cha Skauti Tanzania kinatarajia kuadhimisha miaka Mia Moja  ifikapo Tarehe 21 hadi 29 Julai  Mwaka huu  katika Kampasi ya Chuo Kikuu Makao Makuu Mjini Dodoma kwa kushirikisha Vijana wapatao 5,000 kutoka Wilaya zote za Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na zaidi ya wageni 1,000 kutoka Nje ya Tanzania.


SKAUTI MKUU BI. MWAMTUM MAHIZA AKIZUNGUMZA MBELE YA MAKAMU WA PILI WA RAIS ZANZIBAR
Mkuu wa Skauti Tanzania Bibi Mwamtumu Mahiza alieleza hayo akiuongoza Ujumbe wa Viongozi  Tisa wa Chama hicho Bara na Zanzibar alipokuwa akitoa Taarifa hiyo kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar.

Bibi Mwatumu alisema vugu vugu la maadhimisho hayo limekuja kufuatia ziara ya Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania wa Awamu ya Nne Mh. Mizengo Peter Pinda alipofanya ziara ya kuhudhuria maadhimisho ya Skauti Nchini Uganda Mwaka 2016 na kushawishika na Maadhimisho hayo.

Alisema kutokana na uzito wa maadhimisho hayo Kitaifa yatakayoambatana na maonyesho na mambo mbali mbali Tuzo maalum zitatolewa kwa Marais waliopita pamoja na watu waliofanya ushujaa zaidi katika utekelezaji wa  ujenzi wa Taifa kiuzalendo.

Mkuu huyo wa Skauti Tanzania alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba mipango imeanza kuchukuliwa katika hatua za awali za maadhimisho hayo ambapo Vijana  Kumi wa Skuli za Msingi na Kumi Sekondari wataandaliwa kila Halmashauri za Wilaya Nchini washiriki kwenye tukio hilo muhimu.

Alieleza kwamba Wizara za Elimu, Afya, Mambo ya Ndani, Mambo ya Nje, Tamisemi pamoja na ile inayosimamia Utamaduni kwa upande wa Tanzania Bara zimeshateuliwa  na Waziri Mkuu Mh. Kassim Majaliwa  kusimamia  jambo hilo la Kihistoria.

Bibi Mwatumu alifahamisha kwamba Mataifa Manne ya Kigeni ambayo ni Korea, Poland, Uganda, na Malawi yameshathibitisha kuhudhuria Maadhimisho hayo.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haina pingamizi kwa Vijana wake katika kushiriki Maadhimisho hayo ya Miaka 100 ya Skauti Tanzania.

Balozi Seif alisema Skauti ni sehemu muhimu na adhimu kwa kuwaandaa Vijana katika muekeo wa kuwa na Utii, Heshima na Maadili mema, lakini kubwa zaidi ni kujengeka katika mazingira ya kuwa Wazalendo kwa Taifa lao.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliueleza Ujumbe huo wa Viongozi wa Skauti Tanzania kwamba anaiagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar  kutekeleza wajibu wa kulishughulikia suala hilo katika kuwaanda Vijana wa Zanzibar wawe sehemu ya maadhimisho hayo Kitaifa.

Balozi Seif aliupongeza Uongozi huo wa Skauti Tanzania kwa utayari wao wa kuhakikisha lengo la kuanzishwa kwa Chombo hicho muhimu Nchini Tanzania linafanikiwa.

Chama cha Skauti ndani ya Ardhi ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kimeasisiwa Visiwani Zanzibar mnamo Mwaka 1912.



Na. Othman Khamis Ame
  
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

25/5/2017.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni