RAIS John Magufuli amepokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2016, na kumuagiza CAG kufanya ukaguzi wa kina katika sekta ya madini na kubaini mianya yote inayosababisha nchi kukosa mapato makubwa hususani katika misamaha ya kodi, mikataba na ulipaji wa kodi.
Ripoti hiyo iliwasilishwa Ikulu jijini Dar es Salaam na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad katika hafla iliyohudhuriwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, ripoti hiyo imegusa maeneo mbalimbali yakiwemo ukaguzi wa hali ya hesabu za serikali, misamaha ya kodi, ukusanyaji wa kodi na maduhuli ya serikali, uandaaji na utekelezaji wa bajeti, hali ya deni la Taifa, usimamizi wa rasilimali watu, usimamizi wa mali na madeni ya serikali na usimamizi na uendeshaji wa taasisi za umma zikiwemo taasisi muhimu za kifedha na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Profesa Assad alisema pamoja na hatua kubwa iliyopigwa na serikali katika kuzingatia taratibu za fedha, bado kuna mapungufu mbalimbali yaliyoendelea kujitokeza na ameshauri hatua zichukuliwe kukabiliana nayo ikiwemo kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha za umma katika madini, kuiepusha Tanesco kununua umeme wa gharama kubwa, matumizi mabaya ya misamaha ya kodi na kuongeza mashine za kutoa risiti (EFDs).
Akizungumza baada ya kupokea ripoti hiyo, Rais Magufuli ameipongeza Ofisi ya CAG kwa kazi nzuri inayofanya na ameahidi kuwa serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na ofisi hiyo ili kukabiliana na mianya yote inayosababisha upotevu wa fedha za umma.
Hata hivyo, Rais Magufuli alimuagiza CAG kufanya ukaguzi wa kina katika sekta ya madini na kubaini mianya yote ambayo inasababisha nchi kukosa mapato makubwa hususani katika misamaha ya kodi, mikataba mbalimbali na ulipaji wa kodi.
“Haiwezekani Watanzania wanakosa dawa hospitali wakati dhahabu zao zinaondoka, Watanzania wanakosa maji wakati dhahabu zao zinaondoka, Watanzania wanakosa umeme wakati dhahabu zao zinaondoka, Watanzania wanakosa barabara wakati dhahabu zao zinaondoka, nataka ukakague kwa kina hii sekta ya madini ili Watanzania wajue chao nini na kama kinapatikana sawasawa?” alisisitiza Rais Magufuli.
Aidha, Dk Magufuli pia amemuagiza Waziri Mkuu, Majaliwa kuitisha kikao cha pamoja kitakachomkutanisha CAG na mawaziri wote, makatibu wakuu wa wizara zote, Gavana wa Benki Kuu na wakuu wa taasisi za umma ili kila mmoja aambiwe hali ya hesabu katika taasisi yake na kuchukua hatua.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu ukaongoze hicho kikao na wewe CAG uwaambie kila mmoja katika eneo lake juu ya dosari zake, sitaki kuona dosari zinajirudia zilezile kila wakati,” alifafanua Rais Magufuli.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, CAG anapaswa kuwasilisha ripoti ya hesabu za Serikali kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kabla ya Machi 31 ya kila mwaka, na baada ya hapo ripoti hiyo huwasilishwa katika Bunge kwenye mkutano unaofuata.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni