
Na: Lilian Lundo - MAELEZO.
Maonesho ya ukakamavu na mbinu za medani katika kupambana
na adui hasa kulinda amani ya nchi yetu kutoka Kikosi Maalum cha
Makomandoo wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), itakuwa ni sehemu ya
shamrasha zitakazopamba maadhimisho ya miaka 53 ya Muungano
yatakayofanyika kwa mara ya kwanza mjini Dodoma Aprili 26 mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Watu Wenye Ulemavu,
Jenista Mhagama maadhimisho hayo yanatarajiwa kuhudhuriwa na Rais Dkt.
John Pombe Magufuli, pia yatapambwa na burudani nyingine kutoka vikundi
mbalimbali.
Taarifa ya Waziri Mhagama ametaja shughuli nyingine
zinazotarajiwa kufanyika siku ya Muungano kuwa ni gwaride la heshima
lililoandaliwa na vikosi vya ulinzi na usalama (JWTZ,JKT, Polisi na
Magereza) na onesho la mbwa na farasi waliofunzwa.
Aidha, Waziri Mhagama aliongeza kuwa mambo mengine
yatakayofanyika ni gwaride la uzalendo la wanafunzi wa shule za
sekondari za Dodoma, burudani za vikundi vya ngoma za asili kutoka
Dodoma na Zanzibar, Yamoto Band, vikundi vya muziki wa kizazi kipya
kutoka kwa wasanii Mchungaji Zayumba, Jacob Beats, Mwenge Jazz Band na
Mgosi Maturumbeta.
“Kauli mbiu ya sherehe za kutimiza miaka 53 ya Muungano
wa Tanganyika na Zanzibar ni Miaka 53 ya Muungano; Tuulinde na
Kuumarisha, Tupige Vita Dawa za Kulevya na Kufanya Kazi kwa Bidii,”alifafanua Waziri Jenista Mhagama.
Ametoa wito kwa wananchi wote nchini kusherehekea siku hiyo
muhimu kwa kudumisha amani, upendo, umoja na mshikamano kwa maendeleo
ya nchi.
“Ninaomba kuchukua nafasi ya pekee kuwaomba wananchi
wote waliopo Dodoma kujitokeza kwa wingi uwanja wa Jamhuri siku hiyo ya
Jumatano tarehe 26 Aprili 2017 kuanzia saa 12:00 asubuhi ili
kusherehekea kwa pamoja maadhimisho hayo muhimu kwa nchi yetu,” alisema Jenista Mhagama.
Maadhimisho ya Muungano yanafanyika kwa mara ya kwanza
Dodoma ikiwa ni siku kadhaa tangu Serikali ya Awamu ya Tano ianze
kutumiza azma ya kuhamia katika makao makuu hayo mapya
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni