Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
TAASISI ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa
mara nyingine tena imefanya upimaji wa moyo wa mtoto aliye tumboni mwa
mama yake, kuchunguza magonjwa mbalimbali ya moyo.
Upimaji huo umefanywa katika taasisi hiyo na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Watoto wa JKCI, Naiz Majani.
Akizungumza na waandishi wa habari, Dk. Naiz amesema kuna faida lukuki iwapo mjamzito ataamua kufanya kipimo maalumu.
"Tunatumia Ultra sound kama kawaida kufanya kipimo
hiki, lakini inakuwa ina tofauti kidogo... hatutumii mionzi yoyote,
hivyo hakuna madhara anayoweza kuyapata mama au mtoto wake aliye
tumboni," amesema.
Ametaja faida hizo kuwa ni kupunguza idadi ya vifo
vya watoto wanaozaliwa na magonjwa ya moyo, na kuwaondoa kwenye
masumbufu wanayoweza kuyapata kutokana na kuchelewa kupata matibabu.
"Kwa mara ya kwanza tuliwafanyia kipimo hicho
wajawazito 25 mwishoni mwa mwaka jana ambapo watano kati yao mimba zao
zilikutwa na matatizo.
"Wajawazito hao wanatarajiwa kujifungua wakati wowote
kuanzia sasa na watoto hao wataanza kufuatiliwa kwa ukaribu na kupewa
matibabu ya haraka," amesema.
Amesema waliamua kuanza kufanya kipimo hicho baada ya
kugundua watoto kadhaa hufikishwa katika taasisi hiyo wakiwa katika
hatua mbaya kiasi cha wao kushindwa kuwapatia matibabu.
Amesema inakadiriwa katika kila watoto 100 wanaozaliwa nchini mmoja anakuwa amezaliwa na magonjwa ya moyo.
"Mwaka jana inakadiriwa walizaliwa watoto milioni
moja, kwa msingi huo watoto wapatao 12,000 walizaliwa na magonjwa haya
lakini tuliowaona kliniki yetu ni kati ya 700 hadi 750 pekee," amesema.
"Kuna baadhi ya magonjwa ya moyo yanatakiwa kutibiwa mapema, lakini wanakuja umri umeshakwenda tunashindwa kuwasaidia," amesema.
Mkurugenzi wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi amesema dhumuni kubwa la kuanzisha huduma hiyo ni kugundua matatizo hayo mapema.
"Tunahamasisha kina mama wajitokeze, Tanzania sasa
imepiga hatua kubwa, tunafanya hivi kwa sababu asilimia 85 ya wagonjwa
tunaowafanyia upasuaji ni watoto. Na hawa ndiyo tunaowategemea kuwa Taifa la kesho,
tusipowagundua na kuwatibu mapema maana yake ni kwamba watakuja kuwa
mzigo kwa Taifa miaka ijayo," amesema.
Amefafanua kwamba miaka ya nyuma si kwamba magonjwa
ya moyo hayakuwapata watoto bali hayakuweza kugundulika kutokana na
uhaba wa wataalamu, vifaa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni